Familia moja katika Kaunti ya Murang’a imelazimika kuzika mgomba wa ndizi badala ya mwili wa mpendwa wao, baada ya hospitali moja ya kibinafsi kukataa na mabaki yake ikidai bili ya Sh1.3 milioni.
Kisanga hicho kilitokea Jumamosi ya Desemba 9, 2023 katika kijiji cha Kamuiru kilichoko katika eneobunge la Maragua, wenyeji wakiitaka hospitali hiyo sasa kufanya itakavyo na maiti ya mwendazake.
Mwili wa Bi Irene Wanjiru, 55 ulikuwa tayari umetolewa kutoka hospitali hiyo na kuwasilishwa hadi Mochari ya hospitali ya Maragua tayari kuandaliwa mazishi lakini kukatolewa ilani usikabidhiwe familia hiyo kabla ya ilipe bili hiyo.
Kwa mujibu wa mwanawe marehemu, Bw Mwangi Irungu, mwendazake alianza kusumbuliwa na mwili mwaka uliopita, 2022 na hali ikamzidia Julai 2022 ambapo alilazwa katika hospitali ya kibinafsi iliyoko Kaunti ya Kirinyaga.
“Mamangu aligunduliwa kuwa na Saratani ya kichwa na baada ya kufanyiwa upasuaji na kushughulikiwa katika fani zinginezo katika hospitali hiyo ya Kerugoya, bili yote ilijumlishwa kuwa Sh3.8 milioni,” akasema.
Bw Irungu aliongeza kuwa; “Tulifanya bidii kupitia kuchangisha na tukafanikiwa kulipa Sh2.5 milioni na ndipo tukaafikiana na wasimamizi wa hospitali hiyo kwamba tungepewa ruhusa ya kuzika mwili”.
Alisema kwamba maelewano yalikuwa familia ya marehemu itafute pesa kidogo zaidi ili ikubaliwe mwili uzikwe.
“Lakini baada ya kuchangisha pesa zingine na tukapata Sh80, 000 ambazo tuliwasilisha kwa hospitali hiyo, hali ambayo ilitufanya tupewe mwili tusafirishe hadi mochari iliyo karibu na kwetu, siku ya mazishi tulipigwa na butwaa kuambiwa kwamba tumenyimwa ruhusa ya kuandaa maziko hayo,” akasema.
Alisema kwamba kuna jamaa na marafiki ambao tayari walikuwa wamesafiri kutoka kila pembe ya taifa ili kuhudhuria mazishi hayo, lakini baada ya kufahamishwa kuhusu utata huo wa bili, wakaamua kuandaa mazishi ya mgomba wa ndizi.
“Tulikuwa tumechimba kaburi na katika mila zetu za jamii ya Agikuyu, huwezi ukaacha kaburi likiwa wazi na pia huwezi ukalijaza mchanga bila ya mwili ulionuiwa kuzikwa,” akasema Mzee Nduati Kariga, 87.
Mzee Kariga alisema kwamba kuthubutu kujaza kaburi mchanga bila mwili ulionuiwa kuzikwa, ni sawa na kulaani ukoo mzima wa mwendazake.
Alisema, “Katika hali hiyo, mgomba wa ndizi ndio huzikwa ili kusimamia mwili wa mwendazake na pia kutakasa ukoo wake kwa mujibu wa mila na desturi”.
Alifafanua kwamba mgomba huo hutafutwa ukiwa na mizizi yake ili hata baada ya kuzikwa, utapambana na kisha kuzalisha migomba mingine “hali hii ikiangazia kustawi kwa familia ya mwendazake hata baada ya dhiki ya msiba”.
Aliongeza kuwa mgomba huzaa ndizi ambayo hutumika kama chakula hasa kwa watoto wachanga “na hiyo ni ishara ya kustawi kwa vizazi hata baada ya maziko hayo ya mgomba”.
Familia hiyo ilisema kwamba ikiwa hospitali hiyo inataka kumiliki mwili wa marehemu iko huru sasa kufanya hivyo.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!