Jina la marehemu laitwa kutunukiwa astashahada Mzumbe

Kuitwa kwa jina la aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe – Ndaki ya Mbeya, Yoakim Ndunguru, ili atunukiwe cheti katika mahafali ya 22 ya chuo hicho, kumewatoa machozi watu waliohudhuria shughuli hiyo.

Mkuu wa Chuo hicho, Dk Ali Mohamed Shein alitaja jina hilo ili kumtunuku mwanafunzi huyo, astashahada ya uhasibu, ambapo imeelezwa kuwa Ndunguru alifariki siku chache kabla ya mahafali hayo, baada ya kuugua akiwa likizo.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika leo Novemba 30, 2023 Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Mwegoha amesema mwanafunzi huyo alikuwa amekamilisha kila takwa ili aweze kuhitimu.

“Mkuu wa Chuo (Dk Shein), huyu mwanafunzi ni wa ngazi ya astashahada kozi ya uhasibu ambaye alifariki dunia na alikuwa amekamilisha kila kitu tunaomba kipekee umtunuku cheti,” amesema Mwegoha huku huzuni na simanzi zikitawala kwa wahitimu na wananchi waliojitokeza katika mahafali hayo.

Mwegoha ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi 1,295 wamehitimu mafunzo ya kozi mbalimbali na kwa ngazi tofauti huku akieleza kuwa mafanikio ni makubwa.

“Lakini tumeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi ikiwamo zahanati ya chuo utakaogharimu Sh465 milioni, kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi unaofadhiliwa na benki ya dunia kama mkopo wa Serikali,” amesema.

Akifunga mahafali hayo, Dk Shein amewataka wahitimu kuendelea kujiongezea elimu ili kufungua milango zaidi ya fursa na kujiajiri akieleza kuwa kwa sasa wasomi ni wengi na idadi ya watu inaendelea kuongezeka kuliko ajira.

Amesema Serikali imetimiza wajibu wake kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya chuo hicho na kwamba siku za mbeleni kitapiga hatua kufikia anga za kimataifa.

“Haifai kukata tamaa, bali kujiamini na kujituma ndiyo siri ya maendeleo na dunia ya sasa inahitaji kupambana kwani ajira ni za kupambania, hivyo jiongezeeni elimu ili kufungua milango mingine. Fanyeni tafiti na kubuni teknolojia mpya ambazo zitaendana na wakati wa sasa, ajira zina ushindani na wasomi wanaongezeka,” amesema Dk Shein.

Kwa upande wa mwanafunzi bora chuoni hapo, Rojas Mwalurefu amesema: “Tunamshukuru Mungu aliyetujalia kumaliza masomo yetu, haikuwa kazi rahisi bali uvumilivu, nidhamu na kujituma kuyafikia mafanikio, chuo hiki kimeendelea kutoa wasomi wengi na tunajivunia,” amesema Mwalurefu.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!