Kujifungua kawaida baada ya kujifungua kwa Upasuaji
Ikiwa unajiuliza kama kujifungua kwa njia ya kawaida inawezekana baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji ujauzito uliopita, jibu ni kwamba inawezekana kwa wanawake wengi lakini kuna sababu zitakazo wasaidia wewe na daktari wako kufikia hitimisho kama inawezekana kwako au la.
Usalama kwako na mtoto wako ni jambo muhimu la kuzingatia. Kujifungua kwa kawaida baada ya kujifungua kwa upasuaji sio salama kwa kila mwanamke.
Ikiwa unajaribu kujifungua kwa njia ya kawaida unakuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo, ambayo yanaweza kusababisha utata wa afya ya wewe na mtoto wako- baadhi kuhatarisha maisha. Ndiyo maana ni muhimu kuongea na daktari wako kuhusu hatari hizi.
Ili daktari na wewe kufikiria uwezekano wa kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji, inakubidi wewe na mtoto wako muwe katika afya njema. Unaweza kujaribu kujifungua kwa kawaida hata ukiwa na ujauzito wa mapacha, cha msingi ni daktari kuhakikisha na kusema wote mko katika afya nzuri ya kuhimili zoezi zima.
Sababu hatari ambazo daktari hatakuruhusu kujifungua kwa kawaida baada ya kujifungua kwa upasuaji ujauzito uliopita ni pamoja na:
- Uzito uliopitiliza (kama BMI yako ni 30 au zaidi)
- Shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito (Pre-eclampsia)
- Umri mkubwa (kawaida zaidi ya 35)
- Upasuaji wako wa awali ulifanyika miezi 19 iliyopita.
- Mtoto wako tumboni ni mkubwa sana.
- Kama wakati wa upasuaji ulichanwa kwa wima (vertical cut) hauruhusiwi kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida. Kuna nafasi kubwa ya mshono wako kuachia wakati wa kusukuma mtoto, hali ambayo italeta madhara makubwa kwako na mtoto wako. Itakubidi kufanyiwa upasuaji tena.
Faida za Kujifungua kwa Njia ya Kawaida Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.
Asilimia 70 ya wanawake wanaojaribu kujifungua kwa njia ya kawaida wanafanikiwa, wengine inashindikana kwasababu ya dharura zinazotekea wakati wa kujaribu, wanaishia kufanyiwa upasuaji.
Unaweza kutamani kujaribu kujifungua kwa kawaida baada ya upasuaji kwasababu ya sababu mbalimbali, jaribio hili likifanikiwa kuna faida ambazo ni:
- Hakuna upasuaji utakaofanyika
- Kiasi kidogo cha damu kitapotea
- Uponaji wa haraka
- Inapunguza nafasi ya maambukizi
- Sio rahisi kusumbuka na kidonda kwenye kibofu, utumbo au ogani nyingine.
- Inapunguza nafasi ya kuwa na matatizo makubwa wakati wa kujifungua kwa ujauzito ujao.
Kumbuka
Sio kila hospitali inatoa huduma ya mjamzito kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji katika ujauzito wake wa awali, hivyo katika mpango wako wa kujifungua hakikisha unahusisha hospitali unayotarajia katika mkakati wako ili kujua kama inatoa huduma hiyo. Hata kama nafasi ya mshono uliopita kuachia wakati wa kusukuma ni ndogo, hospitali inatakiwa kujiandaa kwa hali yeyote ya dharura inayoweza kutokea. Baadhi ya hospitali hazina utayari wa vifaa na watu wenye ujuzi kukabiliana na hali ya dharura.
Via:afyatrack
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!