Mabadiliko ya tabia nchi yasababisha kuongezeka kwa magonjwa ya milipuko

MABADILIKO YA TABIA NCHI YASABABISHA KUONGEZEKA KWA MAGONJWA YA MILIPUKO NAKUATHIRI MFUMO WA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA.

Mwandishi wetu
Dubai

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameshiriki katika kikao cha Mabadiliko ya tabia nchi na Afya ngazi ya Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani. Kikao hiki kilichotoa umuhimu wa suala la Afya kilifanyika pembezoni mwa kikao cha 28 cha Duniani kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri Ummy aliuambia mkutano huu kwamba, mabadiliko ya tabia nchi, yamesababisha ongezeko la magonjwa ya milipuko na vifo hususani katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mathalani, magonjwa kama kuhara, malaria, dengue na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama usubi, chikungunya, kichocho, matende na magonjwa ya mfumo wa hewa, magonjwa ya aina hii yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la joto na mvua kubwa au chache zinazoletelezea mafuriko au ukame katika maeneo mbalimbali nchini. Waziri Ummy ametolea mfano wa mafuriko yaliyotokea nchini mkoani Manyara na kupoteza maisha ya watu na wengine kujeruhiwa.

Majanga kama ya mafuriko yameonekana kusababisha milipuko ya ya magonjwa ikiwemo kipindupindu na Homa ya matumbo na kueleza kuwa asilimia 88 tu ya wakazi wa mijini ndiyo wanaopata huduma ya maji safi na salama na kwa upande wa vijijini ni asilimia 77 na watu wenye vyoo vya aina yoyote ni asilimia 98.

Aidha majanga kama ya mafuriko yamepelekea kuharibu vyanzo vya maji na miundombinu iliyopo na kupelekea upungufu na hatimaye milipuko ya magonjwa.” Alisema Waziri Ummy
Tanzania kama moja ya nchi zinazoathirika na mabadiliko ya tabia nchi inaendelea kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuandaa mpango mkakati na miongozo ya kukabiliana na majanga haya katika sekta ya Afya.

Vile vile Wizara imeandaa mfumo wa taarifa unaoweza kubashiri uwezekano wa kutokea milipuko ya magonjwa ya milipuko sambamba na mabadiliko ya hali ya hewa ya kila siku.

Aidha alieleza kuwa Wizara inatafuta fedha za kutekeleza Afua mbalimbali za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na mazingira, Afya na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Dkt.Tedros, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani akihutubia mkutano huu alisema,Viongozi wengi wa nchi duniani wanatambua madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, hata hivyo ipo haja kwa Viongozi wa nchi zetu kutambua uhusiano wa madhara ya kiafya yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuwekeza katika eneo hili.

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la magonjwa kama vile malaria, dengue, nk. Pia, alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikishwa kwa karibu katika kutatua changamoto za majanga ndani ya maeneo yao. Alimalizia kwa kusema janga la mabadiliko ya tabia nchi ni janga la Afya.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!