Ticker

6/recent/ticker-posts

Mpira wa kikapu kuleta amani, maendeleo na ustawi wa jamii



Mpira wa kikapu kuleta amani, maendeleo na ustawi wa jamii.

Ngor Matiang, Mchezaji wa mpira wa Kikapu ambaye pia ni mwanafunzi kutoka Sudan Kusini.

Kwa mara ya kwanza, Umoja wa Mataifa unaadhimisha siku maalum ya mpira wa kikapu ili kutambua mchango wake katika kuleta amani, maendeleo na ustawi wa jamii. Michezo, sanaa na mazoezi yana uwezo wa kubadili mitazamo, tabia, kadhalika kuhamasisha kuondoa vikwazo vya tofauti za rangi na siasa, kupambana na unyanyapaa na pia kumaliza ghasia. Kama michezo miengine ile, mpira wa kikapu unavuka mipaka yote, tamaduni na lugha. Ni kiunganishi kinachowaleta pamoja watu wa asili tofauti kutangamana, kujuana na hatimaye kuchangia kudumisha amani.

Ngor Matiang ni raia wa Sudan Kusini ambaye alingia Kenya mwaka 2012. Anajifunza kucheza mpira wa kikapu na mpaka sasa maisha yake yamebadilika kwasababu ya mchezo huu. Anasema, “Kitu tunafanya mwaka huu ni mpira wa kikapu tu. Baadhi yetu tunategemea mpira wa kikapu na ikiwa mpango wa NBA utafana itakuwa sawa.Kila kitu kitapata suluhu kwasababu ya mpira wa kikapu.Nawasihi wachezaji wenzangu watie bidii na wasivunjike moyo kwani tumeona wengi waliotokea mazingira mabaya lakini sasa wako sawa.Maisha yako sawa juu ya mpira wa kikapu.Yaani napata kila nnachohitaji kwasababu ya mpira wa kikapu…watu wananipenda.”

Vivyo hivyo kwa mchezaji wa kulipwa Hasheem Thabit anayetokea Tanzania na, ”nimecheza mpira wa kikapu kwa miaka kadhaa kwenye ligi ya NBA,nyengine kadhaa dunia nzima.Nimefurahi kusikia Umoja wa Mataifa katika kukuza mchezo wa mpira wa kikapu,katika ustawi wa jamii.Ni hatua kubwa sana kwa mchezo huu na nimefurahi sana kusikia hilo.”

Mpira wa kikapu ni kiunganishi muhimu

Kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la mpira wa kikapu, FIBA, takribani watu milioni 450 kote ulimwenguni wanacheza mchezo mpira huu.Barani Amerika na Ulaya ukiwa na tija zaidi kwenye uchumi wa taifa na pia kwa wachezaji na familia zao.Mwaka 2019, ligi ya mpira wa kikapu barani Afrika ilizinduliwa na kwa sasa timu 12 kutoka mataifa kadhaa ya bara hilo zinashiriki kwenye mchezo huo kwa malipo.Mpira wa kikapu huchezwa na watu kutokea matabaka mbalimbali na majina makubwa kama Michael Jordan, Magic Johson, Kareem Abdul-Jabar, Larry Bird, marehemu Kobe Bryant, Lebron James, Steph Curry yanaupa umaarufu mkubwa.Okuot Majuok ambaye naye pia anatokea Sudan Kusini anakiri kuwa mpira wa kikapu umewapa watu wa nchi yake nafasi ya kubadili maisha kwavile, ”Mpira wa kikapu ni mchezo muhimu.Familia yangu yote inacheza mpira wa kikapu.Hata babangu alikcheza mpira wa kikapu.Sisi raia wa Suda kusini, wengi wetu tunapenda kushiriki kwenye NBA kama vile Manute Bol,Luol Deng …wengi wanacheza huko.Kwahiyo naupenda mpira wa kikapu.”

Hasheem akimulika changamoto nchini Tanzania angependa mchezo wa mpira wa kikapu uwe mkubwa zaidi kwani, ”Mimi kama mimi umenisaidia kujiweka kimaisha binafsi na pia katika jamii imesaidia hilo.Kwahiyo ili mchezo wa mpira wa kikapu uweze kuwa mkubwa Tanzania ,ningependelea kama wangeweza kurejesha michezo mashuleni…sasa hivi naona kama hakuna michezo mikubwa.Kama wangerejesha michezo mashuleni ingesaidia kukuza mchezo wa mpira wa kikapu.”

Ligi ya NBA imetua Kenya

Hapa nchini Kenya, mwezi Septemba mwaka huu wa 2023, Chama cha mpira wa kikapu cha Marekani, NBA, kilitiliana saini na wizara ya michezo makubaliano ya kufungua ofisi yake kwenye mji mkuu Nairobi.

Ofisi hiyo ni ya tano ya NBA barani Afrika kwani nyingine ziko Misri, Senegal, Afrika Kusini na Nigeria. NBA inasimamia ligi inayozileta pamoja timu 30 nchini Marekani. Je,hatua hii imepokewa vipi? Julius Esogo ni mchezaji mpira wa kikapu wa timu ya Langata Barracks jijini Nairobi na anaamini italeta tija na,” Nahisi vizuri kwani kipaji changu kitapata mlezi niweze kwenda nchi nyengine na kushirikiana nao.Sisi wachezaji wa mtaani baadhi ya wakati tunahisi tumetengwa kwahiyo hii ni nafasi muhimu ya kujumuishwa na kutanuka.”

Chini ya makubaliano ya NBA na Kenya, vipaji vitapata nafasi kukuzwa kupitia mpango wa Talanta Hela.Mipango pia ipo ya kuunda miundombinu ya kufanikisha mchezo wa mpira wa kikapu, kuwapatia mafunzo makocha na ujenzi wa uwanja maalum wa kufanyia mashindano. Kwa upande wake,ajenda ya 2030 ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa inaitambua michezo kama kiungo muhimu cha ustawi wa jamii.Julius Esogo amecheza mpira wa kikapu kwa miaka 20 na anaamini kuwa hatua ya Umoja wa mataifa kutenga siku maalum itakuwa na manufaa, ”Mimi najihisi vizuri sana.Kabla nijiunge na timu kubwa nilikuwa nachezea Obama Feba.Hatukua na uzingo,tulitumia kopo la plastiki lililokatwa ili kufunga mabao.Hapa nilipo naamini mambo yatakuwa shwari sasa.”

Mpira wa kikapu una uwezo wa kuleta uwiano na ushirikiano katika sekta mbalimbali za maisha na pia kuwapa nafasi washiriki kutazamana kwanza kama binadamu kisha wachezaji.



Post a Comment

0 Comments