MSD itoe huduma za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwa wateja wao - dkt. jingu

MSD itoe huduma za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwa wateja wao – dkt. jingu

Na. WAF – Morogoro

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameilekeza Bohari ya Dawa (MSD) kuwajali wateja na kuwashirikisha katika suala zima la kuwapa huduma za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za Afya nchini.

Dkt. Jingu amesema hayo wakati akifungua kikao cha ishirini na mbili (22) cha baraza la Wafanyakazi la MSD Mkoani Morogoro ambapo amesisitiza kuwa, kujali wateja ni msingi wa kuwahudumia kulingana na mahitaji yao.

“Ni muhimu sana kuwajali wateja wetu na tuwashirikishe katika suala zima la kuwapa huduma za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za Afya nchini ili wajue kazi inayofanywa na Serikali.” Amesema Dkt. Jingu

Aidha, Dkt. Jingu amesisitiza umuhimu wa MSD kujiendesha kibiashara na kuwa wabunifu ili kuweza kuleta ufanisi na tija katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Mavere Tukai amesema kuwa MSD ni miongoni mwa Taasisi za kimkakati na imeanza kujiendesha kibiashara.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja, MSD imeweza kuongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa za Afya kwa kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji ambapo upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka 51% mwaka jana wa fedha, hadi kufikia zaidi ya 80% mwaka huu.” Amesema Bw. Tukai

Amesema, eneo hili pia linaonekana kwenye kutimiza mahitaji ya wateja ambapo mwaka jana ilikuwa ni asilimia 44 na hii imeongezeka na kufikia asilimia 78.

Kwa upande wa mauzo, Tukai amesema kuna ongezeko la mauzo ya bidhaa za Afya kutoka shilingi Bilioni 77 mwaka jana wa fedha na kufikia shilingi Bilioni 123 mwaka huu wa fedha.

“MSD itaendelea kuboresha kazi zake kwa kuimarisha utendaji wa kazi zake ili kuendelea kutoa huduma za upatikanaji wa bidhaa za dawa kwa Watanzania.” Amesema Bw. Tukai

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!