Watu wanne wamefariki dunia na wengine wanane wamejeruhiwa baada ya kupigwa radi wakiwa wamejikinga mvua kwenye mgahawa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu amesema tukio hilo limetokea jana Desemba 19, 2023 wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Akizungumza leo Desemba 20, 2023, Kamanda Makungu amesema wananchi hao walipigwa radi saa 1.30 usiku katika Kijiji cha Buyezi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Buyezi, Michael Kihunga amesema waliofariki ni Vitus Matalo (26), Phita Meshack (36), Fazol Meshack (46) na mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Itaba, Eslom Nathan (12).
“Walikutwa na mkasa huo wakiwa wamejikinga wasinyeshewe kwenye mgahawa mmoja hapa kijijini. Majeruhi tumewapeleka katika zahanati ya kijiji, baadaye waliruhusiwa hali zao zilipokuwa nzuri,” amesema.
Eliana Daudi na Costansia Lameck, manusura wa tukio hilo wamesema kuwa wakati mvua ikinyesha walisikia ngurumo na ghafla walipoteza fahamu.
Wameeleza walipozinduka muda mfupi baada ya ngurumo walishangaa kusikia wenzao wamefariki dunia.
Desemba 4, 2023, radi iliua watu watano wilayani Masasi mkoani Mtwara.
Radi ni sauti yenye ngurumo kubwa angani ambayo huambatana na mng’aro mkali mithili ya umeme unaotokea wakati mvua inaponyesha.
Umeme unaweza kutokea ama kati ya mawingu yenyewe, kati ya mawingu na ardhi au kati ya mawingu na vitu vingine kama vile miti au majengo.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!