Samia aagiza hatua za haraka kusaidia wahanga wa mafuriko

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameziagiza mamlaka nchini humo kuelekeza nguvu za uokozi na utafiti kwenye eneo la Katesh baada ya mafuriko kusababisha vifo vya watu wapatao 50 kaskazini mwa nchi hiyo.

Vifo vya watu hao pamoja na majeruhi zaidi ya 80 vilitokana na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Jumapili (Disemba 3) na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo kutoka milimani.

Akiwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaofanyika mjini Dubai, Rais Samia alisema amesikitishwa na vifo hivyo na kuagiza “nguvu kubwa ya serikali ielekezwe katika wilaya ya Hanang ili kuwasaidia.” wananchi.

Kulingana na mamlaka za serikali nchini Tanzania, mvua kubwa zilianza kunyesha majira ya saa 11:00 alfajiri ya Jumapili na zikasababisha mafuriko yaliyoporomosha tope kutoka Mlima Hanang, mlima wa Volkano ulio na urefu wa mita 3,418 juu ya usawa wa bahari.

Vifo zaidi viliripotiwa kutokea katika maeneo ya Katesh na Gendabi katika wilaya hiyo ya Hanang, maeneo ambayo yapo karibu na mlima huo.

Mashahidi walioshuhudia maafa hayo waliiambia DW kwamba “watu wengine waliopoteza maisha walisombwa na mafuriko ya mkondo wa maji.

Uwezekano wa vifo kuongezeka

Serikali mkoani Manyara ilisema kulikuwa na uwezekano idadi hiyo kuongezeka kwa sababu juhudi za kutafuta miili mingine zilikuwa bado zinaendelea.

Wakati majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali na vituo vya afya na wanaopata nafuu wanaruhusiwa kutoka, baadhi ya familia zilikuwa zimeripoti kutokuwaona ndugu zao zaidi ya masaa 24 baada ya mafuriko na maporomoko hayo.

Mbali na vifo na majeruhi, kumeripotiwa pia uharibufu wa makaazi, vyombo vya usafiri pamoja na miundombinu ya barabara.

Hadi DW inamaliza kukusanya taarifa hii, hakukuwa na na tathmini rasmi iliyotolewa na serikali ingawa kulingana na mkuu wa mkoa huo, Qeen Sendiga, kikosi cha kupambana na maafa chini ya ofisi ya waziri mkuu tayari kilishawawili kwenye eneo la tukio kwa ajili ya uokozi na tathmini.

Source:dw_swahili

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!