Siku ya maombolezo Jamhuri ya Czech baada ya mtu mwenye silaha kuwaua watu 14

Siku ya maombolezo Jamhuri ya Czech baada ya mtu mwenye silaha kuwaua watu 14

Copyright: Reuters

Jamhuri ya Czech imetangaza Jumamosi kuwa siku ya kitaifa ya maombolezo baada ya mtu aliyejihami kwa bunduki kuwaua watu 14 na kuwajeruhi 25 katika chuo kikuu cha Prague.

Rais Petr Pavel alielezea “masikitiko makubwa” na “hasira isiyomithilika kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia”.

Mshambuliaji huyo, ambaye polisi walisema “ameangamizwa”, anaaminika pia kumuua babake na huenda anahusishwa na vifo vya watu wawili wiki iliyopita.

Ni moja ya matukio mabaya zaidi ya ufyatuaji risasi katika historia ya hivi karibuni ya Uropa.

Tukio hilo lilianza mwendo wa 15:00 saa za ndani (14:00 GMT) siku ya Alhamisi katika jengo la Kitivo cha Sanaa cha Chuo Kikuu cha Charles katikati mwa mji mkuu wa Czech.

Kanda za videoziliibuka baadaye kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi ya watu wakiruka kutoka kwenye kingo za jengo hilo lenye ghorofa kadhaa, huku milio ya risasi ikisikika.

Katika video tofauti, watu waliojawa na hofu wanaonekana wakikimbia eneo hilo maarufu kwa watalii.

Katika kikao kifupi Alhamisi jioni, mkuu wa polisi wa nchi hiyo na waziri wa mambo ya ndani walisema mtu huyo mwenye bunduki alikuwa mwanafunzi katika kitivo hicho.

Sababu za mtu huyokutekeleza shambulio hilo bado hazijabainika.

Taarifa za awali zilidokeza kuwa hakuna afisa wa polisi aliyejeruhiwa katika shambulio hilo, mamlaka ilisema.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!