Tanzia: Mwanafunzi aliyekufa kwa kula uyoga azikwa.
Mchungaji wa Kanisa la EAGT, George Mpambisa akiongoza ibada ya kuaga mwili wa mwanafunzi, Thompson Thomas (18) aliyefariki kwa kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu. Mwili wa mwanafunzi huo umezikwa leo katika makaburi ya Nyasaka jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.
Watu wengine saba waliokula uyoga wanaendelea na matibabu hospitalini.
Mwanza. Simanzi imetawala katika ibada ya kuaga mwili wa mwanafunzi, Thompson Thomas (18) aliyefariki dunia kwa kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu.
Ibada imefanyika leo, Jumatatu Desemba 19,2023 nyumbani kwao Mtaa wa Mabatini Kaskazini jijini Mwanza, ikiongozwa na Mchungaji wa Kanisa la EAGT, George Mpambisa.
Maziko yamefanyika katika makaburi yaliyoko Nyasaka, jijini Mwanza ambapo marehemu alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi wawili waliofariki dunia kwa kula uyoga huo.
Mwili wa mwanafunzi mwingine, Warda Zuberi ulizikwa jana Jumatatu Desemba 18,2023 katika makaburi yaliyopo Mabatini, jijini Mwanza.
Watu wengine saba waliokula uyoga huo katika familia mbili wamelazwa wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Wakati wa kuaga mwili, Mchungaji Mpambisa amewataka wanafamilia, ndugu na jamaa kupokea kifo cha kijana akisema neno la Mungu linaeleza wazi kuwa kila mwanadamu ataonja umauti.
“Kifo cha kijana huyu kimetuuma sana sisi viongozi wa kanisa alilokuwa akisali. Tumuombee apumzike kwa amani na tuifariji familia yake,” amesema.
Pia ametumia msiba huo kuwaonya wanaume wanaotelekeza familia na wanawake wanajiuza badala ya kufanya shughuli halali za kuzalisha kipato.
“Kuna watu wamelea watoto ni wadokozi, wengine ni majambazi, wengine wezi lakini wanasema mimi ni Mkristo. Chukueni hatua Mungu ametupatia nafasi nyingine ya kujirekebisha, huyu mtoto hakuyafanya hayo lakini leo amelala,” amesema na kuongeza:
“Mungu anakuwekea siku nyingi ili pengine utubu, uache dhambi hizo. Tengeneza mambo ya familia yako, acha ulevi, sigara na kuvuta ugoro, acha kuiba na dhambi nyingine,” amesema
Mkazi wa mtaa huo, Helena James amesema kifo cha wanafunzi hao kimewaachia funzo la kutonunua vyakula kiholela badala yake wataongeza umakini ili kuepuka madhara.
“Haikutarajiwa lakini imeshatokea, tumewapoteza hawa watoto, hili ni fundisho kwetu kuwa makini hasa kutonunua chakula kwa wapitanjia,” amesema Helena.
Mama wa mwanafunzi huyo, Eva Thomas, aliyekuwa akibubujikwa machozi tangu mwili wa mwanaye ulipowasili nyumbani kutoka chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Bugando alishindwa kuaga.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!