Ugonjwa wa Mpox waendelea kuisumbua DRC, WHO yasaidia.
Mpox ugonjwa nadra lakini hatari yake ni sawa na virusi vya ndui ambavyo sasa vimetokomezwa.
Kuanzia Januari 1 hadi katikati ya Novemba mwaka huu 2023, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imerekodi zaidi ya wagonjwa 13,000 wanaoshukiwa kuwa na virusi vya Mpox na zaidi ya vifo 600 vimehusishwa na ugonjwa huo.
Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya kila mwaka yaliyoripotiwa ikilinganishwa na kilele cha awali cha zaidi ya wagonjwa 6,000 walioripotiwa mwaka wa 2020.
“Mlipuko huo unaenea kijiografia, ikiwa ni pamoja na mikoa ambayo haikuwahi kuwa na Mpox. Maambukizi ya Mpox yameripotiwa katika kanda za afya 156 kutoka mikoa 22 kati ya 26 (85%).” Ameeleza leo Dkt Rosamund Lewis, Kiongozi wa wataalamu wa Mpox katika shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO alipozungumza na wanahabari hii leo mjini Geneva, Uswisi.
WHO hivi majuzi ilikamilisha kazi nchini DRC kutathmini hali na kuunga mkono mwitikio wa kitaifa. Hii ni hali tata sana, ikizingatiwa kwamba DRC inakabiliwa na masuala mengine ya dharura ikiwa ni pamoja na kipindupindu na migogoro ya kibinadamu.
Wataalamu wa afya wa mashinani na kitaifa wanajitahidi kukabiliana na janga ambalo linaenea kijiografia, na kuongeza kasi ya maambukizi kupitia ngono kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Maambukizi ya ngono ya mpox yamerekodiwa kwa muda, ikiwa ni pamoja na mlipuko wa Nigeria unaoendelea tangu 2017. Ilikuwa njia kuu ya maambukizi katika nchi ambazo zilikumbwa na milipuko endelevu kwa mara ya kwanza mnamo 2022 – na nyingi za nchi hizi zinaendelea kushuhudia maambukizi hadi leo.
Afisa huyo wa WHO ameeleza kuwa kuna haja ya haraka ya kuwekeza katika uwezo wa kutambua, kuthibitisha na kughughulikia. WHO inafanya kazi na Wizara ya Afya ya DRC kusaidia usambazaji wa vufaa vya kukusanya sampuli na kusafirisha, na kuchunguza sampuli kutoka kwa watu wanaoshukiwa huko Kinshasa, Kivu Kusini na maeneo mengine yaliyoathirika. Kwa sasa, ni asilimia tisa tu ya maambukizi ya Mpoksi yamethibitishwa kimaabara.
Dkt. Rosamund Lewis amesisitiza akisema, “Mlipuko wa ugonjwa wa Mpox nchini DRC ni ukumbusho wa haja ya kuendelea kwa ushirikiano na uratibu wa kimataifa ili kudhibiti na hatimaye kukomesha maambukizi ya Mpox kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu. Mapema mwezi huu, WHO iliarifiwa kuhusu mlipuko unaoshukiwa kuwa kwenye meli ya kitalii yenye ratiba kusini-mashariki mwa Asia.
Tunawahimiza watu binafsi, mamlaka za afya za mitaa na waandaaji wa safari za baharini na mikusanyiko mingine mingi kuendelea kushirikishana taarifa, kuongeza ufahamu na kuchukua hatua zote ili kupunguza hatari ya milipuko ya Mpox.”
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!