Chanzo cha ajali ya ndege,Soma hapa

chanzo cha ajali ya ndege 

Zifahamu sababu 5 zinazoweza sababisha ajali ya ndege

Licha ya kwamba abiria wengi wamekuwa na wasiwasi kuhusu ajali za ndege wanapokuwa angani lakini ukweli zimekuwa zikitokea kwa nadra sana.

Watalaam wengi wanautaja usafiri wa ndege kama moja ya usafiri salama zaidi duniani ukilinganisha na usafiri mwingine ukiwemo wa gari unaotumika na wengi.

Hata hivyo, ajali za ndege zimekuwa zikitokea mara kadhaa zikihusisha ndege kibinafsi na zile za kibiashara.

Mnamo Novemba 2022, abiria 19 walifariki katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba nchini Tanzania.

Ukiacha hiyo, zipo ajali nyingi za ndege duniani zilizowahi kutokea zinazothibitisha pasi na shaka sababu zinazoweza kusababisha ajali ya chombo hicho.

Oktoba 2018, ajali ya ya Lion Air Flight 610 Indonesia, iliua watu wote 189 waliokuwemo kama ilivyo kwa Boeing 737 Max, Ethiopian Airlines iliyoua watu wote 157 mwezi machi 2019. Ajali nyingine maarufu ni ya Malaysia Airlines Flight 370 iliyopotea Machi 8, 2014 ikiwa na abiria 227 na wafanyakazi 12.

Ingawa ajali nyingi za ndege zinaweza kuwa na mchanganyiko wa sababu. Na zinaweza kuwa na sababu nyingine mbalimbali lakini sababu za kawaida na kubwa zinazotajwa zaidi ni hizi 5.

1. Makosa ya kibinadamu

Sababu hii inatajwa kuchukua nafasi zaidi, kuliko zingine. Uchovu wa kazi, msongo wa mawazo, kupuuza au kutochukua uamuzi sahihi na wa haraka unaweza kupelekea kufanyika kwa maamuzi hatarishi na kusababisha ajali.

Ndege ya Sriwijaya Air SJ-182 ya Indonesia iliyoanguka Januari 9, 2021 na kuua watu 62, ripoti ya uchunguzi ilitoa sababu mbili zilizosababisha ajali hiyo. Mosi ni tatizo kwenye throttle (kifaa kinachodhibiti mfumo wa mafuta au nguvu ya ingini, lakini pili ni rubani kutochukua hatua ya haraka na sahihi baada ya kuwepo kwa viashiria kadhaa vya hitilafu kabla ya safari.

2. Hitilafu za kiufundi

Makosa ya kiufundi, yanatarajiwa ingawa nayo ni kwa uchache kutokana masharti ya ukaguzi na urushaji wa ndege, ukilinganisha na makosa ya kibinadamu, lakini yanatokea.

Ukiacha ndege ya Sriwijaya Air, unaikumbuka ajali ya ndege iliyoua watu 76 waliokua katika msafara wa timu ya soka ya Chapecoense ya Brazil wakielekea Colombia kucheza mchezo wa fainali ya Sudanmericana dhidi ya Atletico ya Nacional ya Medellin? Sababu yake ilikua ni ya kiufundi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa uwanja wa ndege, marubani waliwaambia ndege hiyo ilikuwa imepata matatizo katika mfumo wake wa umeme.

Na eneo kubwa la kiufundi linalotazamwa zaidi ni uchakavu wa vifaa ama kutofanyiwa marekebisho ya uhakika, haraka na mara kwa mara ya baadhi ya vifaa vinavyohatarisha usalama wa ndege.

3. Matatizo ya hali ya hewa

Kwa mujibu wa Gloria Kulesa kutoka wa Mamlaka ya udhibiti wa anga Marekani, hali ya hewa ni sababu kuu inayochangia karibu 23% ya ajali zote za anga – ikiwa ni pamoja na zile mbaya kubwa na ndogo – kote ulimwenguni.

Hii ni sababu pia lakini wataalam wanaitaja kwa uchache wake ukilinganisha na makosa ya kibinadamu. Mvua kubwa, radi na dhoruba nyinginezo zinazoambatana na upepo au kujijenga kwa barafu kwenye mabawa ya ndege au sehemu ya nyuma ni baadhi ya sababu za hali mbaya zinazozungumzwa.

Wanasema ni nadra sana kwa hali ya hewa peke yake ikasababisha ajali ya ndege.

“Siwezi kufiiria ajali ambayo hali mbaya ya jewa ilikua chanzo cha tatizo”, anasema Sylvia Wringley, rubani na mwandishi wa ‘Why planes crush’ (Kwa nini ndege zinaanguka/zinapata ajali)

Sylvia anasema “lakini yanaweza kuwepo mazingira ambapo hali ya hewa ikaiweka ndege katika hatari ya kupoteza muelekeo”.

Upo mfano, ingawa bado haijathibitishwa wazi kwanini Air Algerie Flight 5017 ilianguka katika jangwa la Sahara mwezi Julai, 2014 na kuua watu wote 118 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, kumekuwa na ripoti kwamba chanzo ni hali mbaya ya hewa.

4. Kupoteza kwa mawasiliano ya rada

Rada ya kuongozea ndege, ndiyo msingi wa urukaji na utuaji wa ndege. Inatoa uelekeo na muongozo kwa rubani kuanzia kupaa na kufuatilia mwenendo wake wakati wote ikiwa angani mpaka kutua.

Ni kiungo cha msingi cha mawasiliano wakati wote wa safari ya ndege iwe ya abiria ama mizigo. Ikiwa kutatokea hitilafu ya mawasiliano baina ya vyombo hivi viwili, uwezekano wa kuiweka ndege kwenye hatari ya kupata ajali ni mkubwa. Imetokea mara kadhaa ndege kupoteza mawasiliano na kupotea. Zingine hazileti madhara zingine zinapotea na kuleta madhara.

Wahudumu wa ndege ya Boeing 777-200ER walidunu na mawasiliano na Air traffic control (ATC) ama rada dakika 38 baada ya kupaa, ikiwa kusini mwa bahari ya China, ikitokea Kuala Lumpur, Malaysia kwenda Beijing, China.

Lakini baadae ya saa moja, ikanaswa na rada ya jeshi kabla ya kupoteza tena mawasiliano na kupotea ikiwa na abiria 239. Ilitafutwa miaka na miaka bila mafanikio, ingawa kuna mabaki katika yameanza kutambuliwa yalikuwa ya ndege hiyo yaliyopatikana sehemu mbalimbali baharini ikiwemo visiwa vya Reunion.

5: Kushambuliwa au kutekwa

Kushambuliwa huku inaweza kuwa ni kwa silaha kama makombora ama viumbe kama ndege wakubwa wa angani.

Kwa viumbe kama ndege mashambulio yake yanaleta madhara kidogo, wapo ndege ambao wamekuwa tishio kwa usalama wa ndege na rubani.

Kampuni moja maarufu ya bima ya Marekani ya Xinsurance inaeleza kuanzia mwaka 1990 mpaka 2020, kulikuwa na taarifa za ndege 74 kuhahiribwa na ndege nchini Marekani pekee hasa ndege ndogo. Nyingi zikiharibika kiasi cha kutofaa.

Kwa upande wa mashambulizi ya kutumia silaha kama makombora, pia si sababu inayotokea sana, lakini ni moja ya sababu inayotajwa. Ndege ya Malaysia Airlines Flight 17 ilidondoka mashariki mwa Ukraine Julai 17, 2014 na watu wote zaidi ya 200 waliokuwemo walifariki, wengi wao wakiwa ni raia wa Uholanzi.

Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Uholanzi mwaka 2015, ilibaini kwamba ilishambuliwa na kombora lililotengenezwa na Urusi. Ripoti nyingine ya uchunguzi ya 2016 iliongeza kuwa washambuliaji walikuwa wapiganaji waliojitenga mashariki mwa Ukraine wanaoungwa mkono na Urusi. Urusi iliiteka Crimea ya Ukraine mwaka 2014.

Via:Bbc

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!