Fahamu aina ya mbwa rafiki kufugwa na hatua za kufuata kabla na wakati wa kuwafuga viumbe hawa

Fahamu aina ya mbwa rafiki kufugwa na hatua za kufuata kabla na wakati wa kuwafuga viumbe hawa.

Mwanza. Wataalamu wametaja sababu za mbwa kumshambulia mmiliki wake au watu wanaomzunguka, wakieleza njia za kuepuka hatari hiyo.

Hayo yanaelezwa zikiwa zimepita siku nne tangu kusambaa taarifa ya mama na watoto wawili, wakazi wa Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza, kunusurika kifo baada ya kushambuliwa na mbwa waliokuwa wakimfuga.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024.

Baba wa familia hiyo, Nicholas Kunju alisema walifuga mbwa wawili, wa jike (pitbull) na  dume (bulldog) kwa takribani miaka saba.

Swali analojiuliza ni nini kilitokea hadi mbwa dume akachachamaa na kuwashambulia watoto na mke wake?

Akijiuliza hayo, kwenye mitandao ya kijamii waliofuatilia habari hiyo waliibua maswali, Je? ni aina gani ya mbwa ni rafiki kufugwa na hatua za kufuata kabla na wakati wa kuwafuga viumbe hao.

Akizungumza na Mwananchi Digital, mtaalamu wa mifugo, Joseph Ndalu amesema sababu za mbwa kuwashambulia wamiliki wake zinatofautiana kulingana na mazingira.

Amesema utamaduni wa kufuga wanyama hao kiholela na kwa mazoea ni sababu kuu.

Ndalu ametaja sababu nyingine kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, kutopewa chanjo na dawa za kuua vimelea wa nje na ndani, ikiwamo minyoo, kutopewa chakula kwa wakati na ujazo unaohitajika, kufanyishwa michezo wasiyoipenda na kuanzisha mazingira hatarishi kwa kiumbe huyo.

“Tunasisitiza wananchi kuwatumia maofisa mifugo waliopo kwenye kila kata ili kupata uelewa wa aina ya mbwa wa kufuga kulingana na mahitaji,” amesema Ndalu.

Aina za mbwa

Ndalu amesema mbwa wamegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni wenye maumbile makubwa na madogo.

Kundi la wenye maumbile makubwa, amesema ndilo hatarishi, linalohitaji umakini mkubwa na tahadhari. Linaundwa na mbwa aina ya Bulldog, Pitbull, Rottweiler na Cane corso.

“Kundi linaloundwa na ‘bulldog’ halihitaji msongo wa mawazo unaochangiwa na kutopewa chakula, matibabu au chanjo kwa wakati. Usipotimiza wajibu huo wana tabia ya kuchukia, hata ukimfungulia anaweza kukushambulia na wakati mwingine ukimkataza hawezi kutii amri,” anasema na kuongeza:

“Ndiyo maana matukio mengi ya watu kushambuliwa na mbwa duniani, ukifuatilia kwa kiasi kikubwa wanaoshambulia ni mbwa jamii ya ‘bulldog’ ambao wanahitaji kutimiziwa mahitaji yao kwa wakati na usahihi.”

Ndalu amewataka wamiliki au waangalizi wa mbwa hao kuhakikisha wanajenga uzio imara ili wasiruke na kuchangamana na kelele za nje.

Anashauri wafunguliwe kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi akieleza muda huo hauna msongamano mkubwa wa watu.

Kuhusu mbwa wenye maumbile madogo (ya kawaida), Ndalu amesema linaundwa na German Sherpherd, Golden Retriever (Scottish) na Belgian Sherpherd, Maltese (wa urembo), Basenji, Kuvinda na wa kawaida (local breed).

“Hawa ni mbwa ambao hawahitaji uangalizi wa hali ya juu hata kama ikitokea changamoto si rahisi kumgeuka mmiliki wake na kumshambulia. Hiyo jamii ya Sherpherd, Basenji na Kuvinda ni mbwa wasikivu na hutumika kwenye ulinzi na uwindaji, pia wanafundishika kwa urahisi,” amesema Ndalu.

Ili kuepuka madhara, mtaalamu huyo ameishauri jamii kufuata kanuni na utaratibu wa ufugaji wanyama kwa kupewa ushauri wa aina ya mbwa na matumizi yake.

Amesema kutofuata utaratibu kunaweza kuleta madhara ikiwemo kusambuliwa na wanyama hao.

Kwa upande wake, Charles Oging’, mtaalamu wa mifugo amesema japokuwa ‘bulldog’ si wakali na wakorofi kulinganisha ‘Rottweiler’ kuna mazingira manne yanayoweza kusababisha wabadilike tabia na hata kuwashambulia wamiliki, watu wanaowatunza na wageni bila kutarajiwa.

“Moja ya sababu zinazoweza kumfanya mbwa kumshambulia mtu yeyote ni ugeni, lakini dume pia wanaweza kubadilika tabia na kumshambulia mtu yeyote anayemsogelea mbwa jike aliye kwenye heat (nyakati za kutunga mimba) kwa sababu ya tabia ya wivu,” amesema.

Mtaalamu huyo amesema maradhi yakiwamo kichaa cha mbwa yanaweza kusababisha mnyama huyo kumshambulia mmiliki, anayemtunza au wageni.

Tukio la Usagara

Nicholas Kunju, mkazi wa Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza, ambaye familia yake ilijeruhiwa kwa kushambuliwa na mbwa aina ya ‘bulldog’ amesema alikuwa dume aliyekuwa akimfuga.

“Familia huwa tunaishi naye pamoja na mtu wa kuwatunza, watoto wangu walirejea likizo kutoka shule, sasa zile movement ‘kutembea’ kwa watoto ndani wale mbwa walihisi upendo umepungua kwao,” alisema Kunju.

Amesema mbwa huyo hakuonyesha dalili za kichaa wala hasira.

“Mtoto mmoja ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne alitoka usiku kufanya shughuli zake nje, yule mbwa dume akamnyemelea na kumtishia, kisha akamshambulia kaka yake,” amesema.

Kunju amesema, “mama watoto wangu aliposikia kelele naye akatoka nje na kuanza kusaidiana na mbwa jike kumdhibiti dume, baadaye wakafanikiwa kuingia ndani na kufunga mlango.”

“Ikabaki fujo nje kwa sababu mbwa wote walibaki wakibweka, ndipo majirani waliposikia na kupiga simu polisi, askari walifika na kuwapiga risasi wakafa ndipo tukaingia ndani kuwapatia msaada wa kuwapeleka hospitali,” amesema Kunju.

Amesema baada ya kupatiwa huduma ya kwanza ya kuchomwa sindano ya kichaa cha mbwa katika Hospitali ya CF, aliipeleka familia yake katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa vipimo vya maambukizi ya vimelea.

“Bugando wamewapima damu kuangalia iwapo kuna maambukizi ya vimelea, tofauti na zile dawa walizochomwa za kichaa cha mbwa, wamepatiwa dawa ya kuchoma kukomesha vimelea hivyo,” amesema.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!