Ticker

6/recent/ticker-posts

Hizi hapa ni Nchi zenye hukumu ya kifo, na Idadi ya watu waliouawa



Hizi hapa ni Nchi zenye hukumu ya kifo, na Idadi ya watu waliouawa

Muuaji aliyepatikana na hatia nchini Marekani anatarajiwa kuwa mtu wa kwanza duniani kunyongwa kwa kutumia gesi ya nitrojeni.

Mwanaume mmoja wa Japan pia amehukumiwa kifo kwa kunyongwa kwa shambulio la uchomaji moto ambalo liliua watu 36 .

Idadi ya watu walionyongwa inaongezeka duniani kote, licha ya nchi nyingi kukomesha matumizi ya adhabu ya kifo.

Ni nchi ngapi zinazotumia adhabu ya kifo?

Kulingana na takwimu za hivi punde zilizokusanywa na Amnesty International , mnamo 2022:

Nchi 55 zilikuwa na hukumu ya kifo

Nchi tisa kati ya hizi zilikuwa na hukumu ya kifo kwa makosa makubwa zaidi, kama vile mauaji mengi au uhalifu wa kivita

Nchi 23 zilikuwa na hukumu ya kifo, lakini hazijaitumia kwa miaka 10

Ni watu wangapi wanauawa kila mwaka?

Data ya Amnesty International ni mchanganyiko wa takwimu rasmi, ripoti za vyombo vya habari na taarifa zinazopitishwa kutoka kwa watu waliohukumiwa kifo na familia zao na wawakilishi.

China haitoi taarifa kuhusu matumizi yake ya hukumu ya kifo.

Ukiondoa Uchina, Amnesty International ilirekodi mauaji 883 ulimwenguni kote mnamo 2022.

Hii ni asilimia 53 zaidi ya watu 579 walionyongwa mwaka wa 2021, na ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu walionyongwa tangu 2017.

Hata hivyo, ni chini sana kuliko takwimu za 1988, 1989 au 2015, wakati zaidi ya watu 1,500 waliuawa katika mwaka mmoja.

Idadi ya hukumu za vifo kote duniani

Idadi ya chini bila kuijumuisha China 1985* hadi 2022

Shirika la Amnesty International linasema takriban hukumu za kifo 2,016 zilitolewa mwaka 2022 katika nchi 52.

Mnamo 2021, nchi 56 ziliweka takriban hukumu za vifo 2,052.

Wafungwa wengi hutumikia kifungo cha muda au hata miongo kwenye hukumu ya kifo kabla ya kunyongwa kwao.

Ni nchi gani zinazotumia adhabu ya kifo zaidi?

Nchi 20 zilinyonga watu mnamo 2022, ikilinganishwa na 18 mnamo 2021.

Amnesty International inaamini kuwa China inatumia hukumu ya kifo kuliko nchi nyingine yoyote. Inafikiriwa kuwaua maelfu ya watu kwa mwaka, lakini hii haiwezi kuthibitishwa.

Kando na China, nchi zilizowanyonga watu wengi zaidi ni Iran, Saudi Arabia, Misri na Marekani.

Nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya hukumu ya kunyongwa

Nchi zenye + zinaashiria idadi ni ya chini

Je, idadi ya watu walionyongwa katika nchi mbalimbali imebadilikaje?

Amnesty International inaangazia nchi 11 duniani ambazo zinaendelea kuwanyonga watu kila mwaka.

Hizi ni pamoja na China, Misri, Iran, Iraq, Saudi Arabia, Marekani, Vietnam na Yemen.

Pia inaamini kuwa Korea Kaskazini “ina uwezekano wa kutumia adhabu ya kifo kwa kiwango endelevu”, lakini haiwezi kuthibitisha hili kwa uhuru.

Nchi ambazo ziliendelea kuwanyonga watu kati ya 2018-2022

Idadi ya walionyongwa nchini Saudi Arabia mnamo 2022 ilikuwa ya juu zaidi kwa miaka 30.

Nchi tano – Bahrain, Comoro, Laos, Niger na Korea Kusini – zilihukumu watu kifo mwaka 2022, baada ya kutotumia hukumu ya kifo kwa miaka kadhaa.

Walakini, idadi ya watu walionyongwa nchini Marekani imepungua tangu kilele cha 1999.

Idadi ya watu walionyongwa nchini Marekani imekuwa ikipungua kwa miongo miwili

Ni watu wangapi wananyongwa kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya?

Amnesty International inasema kulikuwa na watu 325 walionyongwa kwa makosa ya dawa za kulevya duniani kote mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na:

255 nchini Iran

57 nchini Saudi Arabia

11 huko Singapore

Mnamo 2023, Singapore ilimuua mwanamke wa kwanza kwa karibu miaka 20 . Saridewi Djaman alipatikana na hatia ya ulanguzi wa heroin mwaka wa 2018.

Je, ni nchi ngapi zimefuta hukumu ya kifo?

Adhabu ya kifo haitumiki kabisa katika nchi 112, ikilinganishwa na 48 mwaka 1991.

Nchi sita zilikomesha hukumu ya kifo kikamilifu, au kwa sehemu, mnamo 2022.

Nne – Kazakhstan, Papua New Guinea, Sierra Leone na Jamhuri ya Afrika ya Kati – ziliifuta kabisa.

Guinea ya Ikweta na Zambia zilisema itatumika tu kwa uhalifu mkubwa zaidi.

Mnamo Aprili 2023, bunge la Malaysia pia lilipiga kura ya kuondoa hukumu ya kifo ya lazima kwa makosa 11 makubwa ya uhalifu , yakiwemo mauaji na ugaidi.

Bunge la Ghana lilipiga kura ya kukomesha kabisa hukumu ya kifo mnamo Julai 2023.

Je, nchi duniani kote hutekeleza vipi hukumu ya kifo?

Saudi Arabia ndiyo nchi pekee iliyoorodhesha kukata kichwa kama njia ya kunyongwa mnamo 2022.

Mbinu zingine ni pamoja na kunyongwa, kudungwa sindano yenye sumu na kifo kwa kupigwa risasi.

Jimbo la Marekani la Alabama linatarajiwa kumuua muuaji aliyepatikana na hatia anayeitwa Kenneth Smith kwa kutumia gesi ya nitrojeni .

Atakuwa mtu wa kwanza kunyongwa kwa kutumia njia hii. Mawakili wa Bw Smith walitaja njia hiyo ambayo haijajaribiwa kuwa adhabu ya “kikatili na isiyo ya kawaida” .

Alabama na majimbo mengine mawili ya Marekani yaliidhinisha matumizi ya nitrojeni kwa sababu dawa ambazo hutumiwa sana katika sindano za kuua zimekuwa adimu kupata.

Uhaba wa dawa za kutumiwa kwa hukumu hiyo umechangia katika kupungua kwa matumizi ya adhabu ya kifo kote Marekani.

Chanzo:Amnesty International



Post a Comment

0 Comments