Huduma ya kuwapa wanawake ujauzito India

Huduma ya kuwapa wanawake ujauzito India: Jinsi wanaume hawa wa Kihindi walivyonaswa kwenye mtego wa ulaghai

Polisi wanasema wanaume walilaghaiwa kutoa pesa kwa ahadi ya kulipwa vizuri ili kuwapa ujauzito wanawake wasio na watoto.

Ulaghai wa mtandao unavyoboreka, huu ni wa kipekee.

Mapema Desemba Mangesh Kumar (jina limebadilishwa) alikuwa akivinjari kwenye Facebook alipokutana na video kutoka kwa “Huduma ya Ajira ya Wajawazito nchini India” na kuamua kuiangalia.

Kazi ilionekana kuwa nzuri sana kuwa kweli: pesa – na zilikuwa nyingi – kulipwa ili kumpa ujauzito mwanamke.

Ilikuwa, bila shaka, dili nzuri sana kuwa kweli. Kufikia sasa, kijana huyo mwenye umri wa miaka 33, ambaye anapata rupia 15,000 ($180; £142) kwa mwezi akifanya kazi katika kampuni ya mapambo ya sherehe ya harusi, tayari amepoteza rupia 16,000 kwa walaghai – na wanaomba zaidi.

Lakini Mangesh, kutoka jimbo la kaskazini mwa India la Bihar, sio mtu pekee aliyeangukia kwenye mtego wa ulaghai huo.

Naibu msimamizi wa polisi Kalyan Anand, ambaye anaongoza kikosi cha kupambana na uhalifu wa mtandao katika wilaya ya Nawada ya Bihar, aliiambia BBC kwamba kulikuwa na mamia ya waathiriwa wa ulaghai wa kina ambapo wanaume walishawishiwa kutoa pesa zao kwa ahadi ya siku kubwa ya malipo, na usiku katika hoteli na mwanamke asiye na mtoto.

Kufikia sasa, timu yake imewakamata wanaume wanane, kunasa simu tisa za rununu na mashine ya kuchapisha stakabadhi, na bado wanawasaka wengine 18.

Lakini kupata walioathiriwa ni kibarua kigumu zaidi .

“Genge hilo limekuwa likifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na tunaamini limewatapeli mamia ya watu, lakini hakuna hata mmoja ambaye hadi sasa amejitokeza kulalamika, labda kwa sababu ya aibu,” alifafanua.

BBC imeweza kuzungumza na waathiriwa wawili – mmoja alisema amepoteza rupia 799, lakini hakutaka kujadili maelezo zaidi. Mangesh alikuwa tayari kufichua zaidi na, baada ya simu kadhaa, alifichua jinsi alivyotekwa na matapeli.

“Dakika kumi baada ya kubofya video, simu yangu iliita. Mwanaume huyo aliniomba nilipe rupia 799 ikiwa ningetaka kujiandikisha kwa kazi hiyo,” aliniambia.

Mpiga simu – Mangesh anamwita Sandeep sir – alimwambia kuwa atafanya kazi katika kampuni huko Mumbai na kwamba atakapojiandikisha, atatumiwa maelezo ya mwanamke ambaye angempa mimba.

Walimpa rupia nusu milioni – karibu mshahara wa miaka mitatu – ili tu kufanya mapenzi na mwanamke huyo na kuahidi zawadi zaidi ya rupia 800,000 ikiwa angepata mimba.

“Mimi ni maskini, nahitaji sana pesa kwa hiyo niliwaamini,” baba wa watoto wawili wa kiume aliniambia.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizofuata, Mangesh alitakiwa kulipia zaidi ya rupia 16,000 – rupia 2,550 ili kupata hati za mahakama, 4,500 kama amana ya usalama na rupia 7,998 kama Kodi ya Bidhaa na Huduma (GST) kwa pesa alizokuwa akienda kupata.

Amenishirikisha risiti zote na karatasi bandia za mahakama – hati inayoonekana rasmi ina jina lake na ina picha yake pamoja na ya mwanamume aliyevalia sare za polisi. Kwa herufi kubwa kubwa juu, inasema “Mkataba wa Kuzaliwa kwa Mtoto” na maandishi mazuri hapa chini yanasomeka “fomu ya uthibitishaji wa ujauzito”.

Sahihi iliyo mwishoni mwa waraka huo inafanana na ile iliyotumiwa na mtangazaji wa kipindi cha mazungumzo cha Marekani Oprah Winfrey.

Walaghai hao walimvutia kwa kumtumia picha za “wanawake saba-wanane”, wakimtaka achague yule ambaye angependa kumpa ujauzito. “Walisema wangepanga chumba cha hoteli katika mji niliokuwa nikiishi na nitakutana na mwanamke huyo huko,” alisema.

Wakati Mangesh akiendelea kuuliza pesa alizoahidiwa, walimtumia risiti wakisema wameweka akaunti yake ya benki rupia 512,400 lakini pesa hizo zilikuwa zimesitishwa na zingelipwa baada ya kulipa 12,600 kama ushuru wa mapato.

Kufikia wakati huo, Mangesh anasema, alikuwa amepoteza mshahara wa mwezi mzima na aliwaambia kwamba hawezi kulipa tena na akaomba kurejeshewa fedha.

“Lakini Sandeep Sir alikataa na nilipokasirika, aliniambia kwa vile akaunti yangu ya benki ilionyesha mkopo wa rupia 500,000, mamlaka ya kodi ya mapato ingevamia nyumbani kwangu na kunikamata.

“Mimi ni mfanyakazi masikini, nilipoteza malipo ya mwezi mzima na sikutaka kujikuta katika kesi yoyote ya jinai. Niliogopa sana hadi nilizima simu yangu kwa siku 10. Niliiwasha tena siku chache zilizopita,” aliniambia, akiongeza kuwa mwanzoni pia alifikiri nilikuwa sehemu ya genge la matapeli.

Kulingana na DSP Anand, wanaume waliohusika na ulaghai huo ni wasomi – wengine hata wamehitimu – na wanajua jinsi ya kufanya kazi kwa simu za rununu, kompyuta ndogo na vichapishaji. Waathiriwa, kwa upande mwingine, wanatoka pande zote za India na wengi wao wana elimu ndogo.

Mangesh anasema haikumshangaza kwamba huyu anaweza kuwa mdanganyifu kwa sababu “Sandeep sir” alikuwa amemtumia nakala za vitambulisho vyake, ikiwa ni pamoja na moja iliyomtambulisha kama askari wa jeshi la India. Pia aliamini kuwa picha iliyoonyeshwa kwenye Whatsapp ya mpigaji simu – inayoonyesha mwanamke wa kigeni mwenye kuvutia akiwa amembeba mtoto mchanga mikononi mwake – ilikuwa ya kweli.

“Wewe niambie utakosa kuamini hiyo picha?” anauliza.

Polisi wamewakamata wanaume wanane, kunasa simu tisa na printa, na wanawasaka wengine 18 ambao wametoroka

Tatizo ni kwamba, mtaalam wa sheria ya mtandao Pavan Duggal anaeleza, kwamba watu nchini India, “kwa kiasi kikubwa wanaamini sana na mara chache hufanya uthibitishaji huru wa habari kwenye mtandao”, wakipigwa jeki na dhana kujiamini kupita kiasi katika usalama wao.

“Walaghai waliwarubuni kwa ahadi ya pesa za bure na ngono bila malipo ambayo ni mchanganyiko hatari. Katika hali kama hizi, busara mara nyingi hupuuzwa’

Lakini pamoja na ujio wa Covid-19 – wakati huduma ya benki kwa njia ya simu na mtandao ikawa jambo la kawaida – Bw Duggal anasema “zama za uhalifu wa mtandao zilianza” na anaonya kwamba “itaendelea kwa miongo kadhaa”.

Kadiri wahalifu wa mtandao wanavyokuja na mbinu mpya zaidi, za kibunifu na zilizogeuzwa kukufaa zaidi, India italazimika kufanya kazi kwa bidii zaidi kulinda watu kama Mangesh dhidi ya kushambuliwa na walaghai, anaongeza.

“Serikali inahitaji kufanya mengi zaidi ili kujenga uelewa kupitia matangazo ya redio na televisheni kwa kuwa watu wanaiamini serikali zaidi.”

Lakini serikali pekee haiwezi kufikia kila mmoja wa watu bilioni 1.4 wa India.”Idadi ni kubwa mno. Na kutegemea serikali pekee itachukua muda mrefu sana na uchumi wa India utaendelea kudhoofika. Kwa hiyo ni lazima serikali itoe motisha kwa sekta binafsi kujitokeza,” anasema.

Watapeli nao bado hawajakata tamaa kwa Mangesh.

Akizungumza nami kupitia simu wiki iliyopita, “bibi” anapiga. Huyu, alinieleza baadaye, alikuwa mwanamke ambaye alikuwa ameahidiwa kukutana naye.

Siku ya Jumapili usiku, aliniambia kuwa amekuwa akizungumza naye karibu kila siku.

Sasa anamwambia kwamba “Sandeep sir” ndiye tapeli halisi na ameiba kiasi kikubwa cha rupia 500,000 ambazo Mangesh aliahidiwa, lakini bado anaweza kupata rupia 90,000 kama atalipa rupia 3,000 kama GST.

“Nilimwambia sina pesa. Nilimsihi anirudishie pesa zangu lakini akasema haitawezekana. Natamani angalau arudishe rupia 10,000,” aliniambia.

Ninamuuliza ikiwa bado anawaamini matapeli.

“Kwa kweli sijui la kufanya sasa. Nimepoteza malipo ya mwezi mzima na sijaweza kutuma pesa zozote kwa familia yangu huko Bihar. Mke wangu ana hasira sana na hazungumzi nami’.

Ana hasira kwamba “Sandeep sir ” hapokei simu yake tena.

“Wale walionidanganya lazima wapate adhabu ya juu zaidi. Ninafanya kazi ya ngumu ya kuvunja mgongo siku nzima kwa rupia 500. Najua nilifanya makosa makubwa. Lakini walichonifanyia ni makosa sana.”

Via Bbc

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!