Makala: Ufahamu Mmea unaokula Wadudu, Pombe yahusika
Bado tunastaajabia uumbaji wa Dunia na vyote vilivyomo, ambapo leo tunaangazia Mimea inayokula wadudu, yenye Sumu na hata ile yenye neema kwa Wanadamu ambayo mingi kati ya hiyo imekuwa nadra kuonekana na ipo hatarini kutoweka.
Si unajua tena mabadiliko ya matumizi ya ardhi na visa vya Binadamu, wao wanawaza Ujenzi, Ufugaji na kilimo kwahiyo wakiona pori inakuwa vita, lakini hata hivyo Wataalam wa mimea wanasema wanajitahidi kuipanda upya, ili isitoweke.
Mimea hiyo inayokula Wadudu iliyo na umbo la kuvutia, huhitaji ipate maeneo yenye ardhi zenye unyevu ili iweze kustawi na huwa inavutia kuitazama lakini ni hatari kwa viumbe vingine hasa wadudu maana tumezoea Wadudu ndio hula mimea.
Zipo aina nyingi za mimea yenye maajabu mbali na huo unaokula wadudu lakini kwa kuanza tuone huu unaokula wadudu nilioutaja awali, ili kuleta mtiririko mzuri.
1. Venus Flytrap
Huwanasa wadudu kwa majani yake kisha kuwafunika na kuwamengenya kwa kutumia majani yake ambayo ndio huwa mtego kwani anapotua jani hujifunika kwa kasi ya chini ya nusu sekunde.
Baada ya kujifunika mmea huo unaopatikana huko Nchini Marekani hutoa kemikali za kummeng’enya mdudu pole pole ndani ya siku kumi, kisha hujifungua tena kutega windo jipya.
2. Manchineel.
Adui huwa ana mitego mingi sana, si unafahamu hata Chatu humvuta Mbwa kwa urembo wa rangi ya ngozi yake na milio mithili ya miruzi mororo, sasa huu mmea pia una matunda mithili ya Tufaa lakini una sumu kali inayoshangaza na usijaribu kula tunda hilo.
Kwanza una tabia ya kutoa maji maji ya rangi ya maziwa unapougusa, hivyo utomvu wake ukikupata hukusababishia vidonda mithili ya mtu aliyemwagiwa maji ya moto.
Aidha, inashauriwa ukiona mmea huu na mvua inanyesha basi usiusogelee, kwani matone ya mvua yakichanganyikana na utomvu wake yakakuangukia mwilini, basi yatakusababishia madhara makubwa.
Mmea huo, pia inasemekana ukichomwa moto moshi wake ni sumu kali na huweza kumtia mtu upofu na matatizo ya kupumua. Ngoja nikupe usaidizi toka ‘Cuba’ ukiwa porini usiharakie mambo kama ni Tunda watazame Ndege, Wadudu au Nyani wanachokula nawe tumia hicho hicho, ondoa ujuaji.
3. Mimosa Pudica
Sina shaka hata wewe umewahi kutana na majani ambayo ukiyagusa tu, yanasinyaa muda huo huo na baada ya muda hurudia hali yake ya kawaida, huo mmea sasa ndio unaitwa Mimosa pudica.
Kile kitendo cha kusinyaa ni njia ya kujikinga na maadui wala nyasi na waharibufu, maana mdudu anapotua jani likisinyaa atadondoka na mla majani akiona limesinyaa anaweza ghaili kula na kuepa kando kutafuta jani mbadala.
4. Relfessia Arnoldii
Hili ni ajabu jingine, inasadikika kuwa huu ndio mmea wenye maua makubwa zaidi duniani, kwani ua lake lina upana wa mita moja na pia hauna shina, majani wala mizizi.
Unapatikana maeneo Sumatra na Borneo nchini Indonesia, na inaarifiwa kuwa mmea huu hutoa harufu mbaya, kali na inayokera mithili ya harufu ya mzoga.
Kitendo hicho hufanywa ili wadudu waharibifu au shughuli za binadamu zisiendelee jirani na ulipo lakini si unajua tena binadamu, hashindwi kitu kwani aliugundua na kuufanyia utafiti kama kawaida.
5. Mianzi.
Mikoa ya nyanda za juu kusini hapa Nchini mmea wa mianzi hupatikana kwa wingi, mmea huu umewanufaisha wajasiriamali mbalimbali ambao waliamua kutumia rasilimali hiyo kuanzisha usindikaji wa Pombe ya ulanzi.
Ipo hivi: Pombe ya Ulanzi iligunduliwa wakati wa utawala wa Machifu wa kabila la Wabena Wilayani Njombe baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu (ulafi mbaya sijui nani alionja).
Sasa tangu wakati huo, pombe hiyo imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa Mkoa wa Iringa na tayari imesambaa na kufika katika maeneo mengi hasa kusini mwa Tanzania.
Mmea huu ni chanzo cha mapato, ni faida na pia ni chanzo cha migogoro (watu wakilewa wanaanzisha visa si unajua tena).
Mbali na Pombe ya Ulanzi pia shina la Mmea huu hutumika kwa kujengea na kuezekea nyumba. una faida nyingi kuliko hasara lakini ni moja kati ya mmea ambao umekuwa ukijadiliwa sana na Wanadamu.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!