Mambo 6 ya kuzingatia ufanyapo mazoezi barabarani

Mambo 6 ya kuzingatia ufanyapo mazoezi barabarani

Tukio la Jumamosi Juni 22, 2023, watu sita walifariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari ndogo, wilayani Ilemela mkoani Mwanza walipokuwa wanafanya mazoezi pembezoni mwa barabara.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya aliviambia vyombo vya habari, gari hiyo iliyotokea nyuma ilipoteza mwelekeo kutokana na mwendokasi na kusababisha maafa miongoni mwa wakimbiaji 27, na kisha dereva kutokomea kusikojulikana.

Katika baadhi ya miji duniani, zipo njia maalumu – wafanya mazoezi huzitumia. Njia hizo haziruhusu vyombo vya moto kupita, zaidi ya watembea kwa miguu. Na kuufanya usalama wa wale wanaofanya mazoezi kuwa mkubwa.

Kupunguza uwezekano wa kutokea ajali iwapo unafanya mazoezi ya kukimbia katika barabara inayotumiwa na vyombo vya moto, kama magari; kuna mambo sita muhimu unayopaswa kuyazingatia.

1. Tumia eneo la watembea kwa miguu

Barabara nyingi hata zile zinazopatikana katika nchi masikni, zina eneo kwa ajili ya wanaotembea kwa miguu. Eneo hili hutofautishwa na barabara kuu kwa kuchorwa mstari au hutenganishwa na mtaro wa maji katikati.

Kwa sababu za kiusalama ni bora kutumia njia hiyo ikiwa ipo, kuliko kutumia ile yenye magari. Ni salama zaidi kwa sababu haina pisha pisha za vyombo vya moto, hasa ukiwa unafanya mazoezi peke yako au mkiwa wachache.

2. Kimbia upande wa kulia;

Ikiwa mazoezi yako yanakulazimisha kutumia barabara ile ile inayotumiwa na magari, labda kwa kukosekana zile barabara za watembea kwa miguu, Kamanda wa Kikosi cha usalama barabarani, Ramadhani Ng’anzi anakusisitiza utumie upande wa kulia.

‘‘Hii itakusaidia kuyaona magari yanayokuja, itakusaidia kuepuka hatari na kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Wakati huo huo hakikisha ukiwa kulia mwa barabara kimbia pembeni kabisa, epuka eneo la katikati,’’ anasema Kamanda Ng’anzi.

3. Uchaguzi wa mavazi

Kuna nguo ambazo ni rahisi kuonekana ukiwa mbali na nyingine ni vigumu kuonekana. Uchaguzi wa nguo za kuvaa kwa ajili ya mazoezi ni jambo muhimu kwa usalama wa mkimbiaji.

Ikiwa anga ina mawingu, nguo nyeusi sio uchaguzi mzuri. Uchaguzi wa nguo unakuja kwa kuzingatia mandhari au hali ya hewa ya eneo unalokimbia. Vaa nguo ambazo ni rahisi kuonekana na madereva wa magari.

4. Bendera mbili

Hizi ni bendera za rangi maalumu, zinawasaidia wafanya mazoezi kuweza kuruhusu gari ipite au wakati mwingine kuisimamisha gari panapohitajika kufanya hivyo. Ni rangi ya kijani na nyekundu.

Iddi Omari, mfanya mazoezi barabarani kutoka wilaya ya Temeke, ameiambia BBC, ‘‘bendera nyekundu tunatumia kutoa onyo ama kuzuia au kusimamisha gari. Kijani inatumika kusiruhusu gari zitembee baada ya kuzisimamisha au ziendelee na safari.’’

5. Usiweke vifaa vya muziki masikioni au Earphones

Kusikiliza muziki na kufanya mazoezi ni utamaduni wa kisasa. Kwa baadhi ya watu muziki huwasaidia kuongeza morali wakati wa mazoezi. Lakini ni hatari ikiwa unasikiliza muziki eneo lisilo sahihi.

Uwapo barabarani ni muhimu kutoweka vifaa vya kusikiliza muziki masikioni, hilo litahatarisha uwezo wako wa kusikia honi za magari. Unaweza kusikiliza muziki ikiwa eneo unalofanya mazoezi sio bararani.

6. Shiriki Semina

‘Elimu huondoa ujinga,’ Jeshi la Polisi nchini Tanzania huandaa semina kwa wafanya mazoezi barabarani. Hizi ni semina muhimu kuhudhuria kwa wale wanaoshiriki mazoezi ya aina hiyo. Semina hizo hutoa mafunzo ya namna ya kutumia barabara na namna ya kushughulika na madereva.

Baada ya hayo, Kamanda Ng’anzi anashauri kutumia viwanja vya kufanya mazoezi au kufanya mazoezi katika maeneo yenye viwanja – ikiwa hakuna ulazima wa kuingia barabarani. Viwanja ni salama zaidi kuliko barabara.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!