Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yatoa sababu kuwapo joto kali
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yatoa sababu kuwapo joto kali.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tathmini ya hali ya joto na mwenendo wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tathmini ya hali ya joto ya mwaka 2023, ambapo wastani wa ongezeko la dunia kwa mwaka huo ulifikia nyuzi joto 1.40C.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa leo Januari 3,2024 imesema ongezeko la joto hilo limevunja rekodi na kuwa ni mwaka wenye joto zaidi katika historia ya dunia, ukichagizwa na uwepo wa El Nino na mabadiliko ya tabianchi.
Taarifa hiyo imesema kwa upande wa Tanzania tathmini zinaonyesha wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulikuwa nyuzi joto 1.00C na kuufanya mwaka huo kuvunja rekodi ya kuwa na joto zaidi katika historia.
“Ongezeko la joto nchini husababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo mbalimbali.
“Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa Novemba na likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa),” TMA imesema.
Katika kipindi cha Desemba mwaka 2023 kumekuwa na ongezeko la joto kwa baadhi ya maeneo nchini, hususani nyakati ambazo kumekuwa na vipindi vichache vya mvua.
Desemba 29 mwaka 2023 kituo cha Morogoro kiliripotiwa kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 33.9 °C ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 1.3 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi huo.
Kwa upande wa kituo cha Tanga Desemba Mosi 2023 kiliripoti nyuzi joto 33.6 °C ni ongezeko la nyuzi joto 1.5 na Desemba 19,2023 Dodoma ni nyuzi joto 33.5 °C sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.9.
TMA inasema Desemba 2 mwaka 2023 Dar es Salaam ilikuwa na nyuzi joto 33.2 °C ni ongezeko la nyuzi joto 1.2 na Zanzibar nyuzi joto 33.4 °C sawa na ongezeko la nyuzi joto 1.6.
Hata hivyo katika kipindi cha Januari, 2024 vipindi vya mvua vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika maeneo mengi nchini, hali itakayosababisha kupungua kwa joto katika baadhi ya maeneo wakiwamo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!