Amy na Ano ni mapacha wanaofanana, lakini baada tu ya kuzaliwa walichukuliwa kutoka kwa mama yao na kuuzwa kwa familia tofauti.
Miaka kadhaa baadaye, walijuana kwa bahati kupitia onyesho la vipaji la Runinga na video ya TikTok.
Wamesafiri kutoka Georgia hadi Ujerumani, kwa matumaini ya kupata kipande kilichokosekana cha maisha yao. Hatimaye wanakutana na mama yao mzazi.
Kwa miaka miwili iliyopita walikuwa wakitafuta jawabu. Walipokuwa wakitafuta ukweli, waligunduua kuna maelfu ya watu wengine huko Georgia ambao pia walichukuliwa kutoka hospitalini wakiwa watoto wachanga na kuuzwa.
Licha ya majaribio rasmi ya kuchunguza kilichotokea, bado hakuna mtu ambaye ameshikiliwa.
Mwanzo wa Kutafutana
Hadithi ya jinsi Amy na Ano walivyojuana ilianza wakiwa na umri wa miaka 12. Amy Khvitia alikuwa katika nyumba ya mamake mlezi karibu na Bahari Nyeusi akitazama kipindi anachokipenda zaidi cha TV, Georgia’s Got Talent.
Kulikuwa na msichana anaecheza dansi ya jive ambaye anafanana naye.
“Watu wakampigia simu mama yangu na kumuuliza; kwa nini Amy yuko katika mashindano na anatumia jina jingine?'” anasema. Lakini familia yake ilipuuza.
Miaka saba baadaye, Novemba 2021, Amy alichapisha video yake akiwa na nywele za buluu na nyusi zake kabotoa kwenye TikTok.
Maili mia mbili (320km) Tbilisi, mtoto mwingine wa miaka 19, Ano Sartania, alitumiwa video hiyo na rafiki yake. Aliona ni jambo zuri kumtumia kwa sababu anafanana naye.
Ano alijaribu kumtafuta msichana huyo mtandaoni lakini hakumpata, hivyo akaweka video hiyo kwenye kundi la WhatsApp la chuo kikuu ili kuona kama kuna yeyote angeweza kumsaidia.
Mtu aliyemfahamu Amy aliona ujumbe huo na kuwaunganisha kwenye Facebook. Papo hapo Amy alijua Ano ndiye msichana aliyemuona miaka iliyopita kwenye Georgia’s Got Talent.
“Nimekutafuta kwa muda mrefu!” alimtumia ujumbe. “Mimi pia,” alijibu Ano.
Kuonana uso kwa uso
Wote wawili walizaliwa katika hospitali ya uzazi ya Kirtskhi – ambayo haipo tena – magharibi mwa Georgia, kulingana na vyeti vyao vya kuzaliwa, siku zao za kuzaliwa zilitofautiana kwa wiki kadhaa.
Wana mambo yanayofanana. Wote wanapenda muziki, wanapenda kucheza na mitindo yao ya nywele inafanana. Kadhalika waligundua wote wana ugonjwa wa vinasaba wa mifupa unaoitwa dysplasia.
Walipanga kukutana wiki moja baadaye. Amy aliposhuka katika lifti kwenye kituo cha treni cha chini ya ardhi cha Rustaveli huko Tbilisi, yeye na Ano walionana uso kwa uso.
“Ilikuwa kama kujiangalia kwenye kioo, uso ule ule, sauti ile ile. Mimi ni yeye na yeye ni mimi,” anasema Amy.
“Sipendi kukumbatiwa, lakini nilimkumbatia,” anasema Ano.
Waliamua kuzungumza na familia zao na kwa mara ya kwanza wakaelewa ukweli. Waliasiliwa na familia tofauti, kwa tofauti ya wiki mwaka 2002.
Amy alikasirika na kuhisi maisha yake yote yamekuwa ya uwongo. Wakichimba zaidi, mapacha hao waligundua maelezo ya vyeti vyao rasmi vya kuzaliwa, ikiwemo tarehe waliyozaliwa, hayakuwa sahihi.
Mama zao Walezi Wazungumza
Kwa kuwa hawezi kupata mtoto, mama yake Amy anasema rafiki yake alimwambia kuna mtoto asiye na wazazi katika hospitali ya eneo hilo. Atatakiwa kuwalipa madaktari na amchukue nyumbani na kumlea kama wake.
Mama yake Ano naye alisimuliwa hivyo hivyo. Hakuna hata familia moja kati ya walioasili iliyojua kuwa watoto hao walikuwa mapacha, licha ya kulipa pesa nyingi kuwaasili mabinti zao. Wanasema hawakutambua ni kinyume cha sheria.
Hakuna familia iliyofichua ni kiasi ngapi ililipa. Mapacha hao hawakujua ikiwa wazazi wao waliowazaa waliwauza kwa makusudi kupata pesa au la.
Kumtafuta Mama Mzazi
Amy aliamua kumtafuta mama yao mzazi ili kujua ukweli, lakini Ano hakuwa na uhakika kama anataka kuonana naye. “Kwa nini unataka kukutana na mtu ambaye alitusaliti?” Aliuliza.
Amy alitumia kundi la Facebook lililojitolea kuunganisha familia za Georgia na watoto wanaoshukiwa kuasiliwa kinyume cha sheria wakati wa kuzaliwa na alichapisha mkasa wao.
Msichana mmoja nchini Ujerumani alijibu akisema mamake alijifungua watoto mapacha wa kike katika Hospitali ya Wazazi ya Kirtskhi mwaka wa 2002 na aliambiwa wamefariki, lakini sasa ana mashaka.
Vipimo vya DNA vilifichua kuwa msichana huyo kutoka kundi la Facebook alikuwa dada yao, na alikuwa akiishi na mama yao mzazi, Aza, nchini Ujerumani.
Amy alitamani sana kukutana na Aza, lakini Ano alikuwa na mashaka. “Huyu ni mtu ambaye alikuuza, hatakuambia ukweli,” alionya. Hata hivyo alikubali kwenda Ujerumani na Amy.
Katika hoteli huko Leipzig, Amy na Ano wanajiandaa kukutana na mama yao mzazi. Ano anasema amebadili mawazo yake na anataka kuondoka. Lakini baada ya kuvuta pumzi ndefu, anaamua kusonga mbele.
Mama yao mzazi, Aza, anasubiri kwa wasiwasi katika chumba kingine.
Amy anafungua mlango kwa kusitasita na Ano yuko nyuma yake, nusura amsukume dada yake ndani ya chumba. Aza anatembea na kuwakumbatia, pacha mmoja kila upande. Dakika zinapita za kukumbatiana, hakuna anayeongea.
Machozi yanatiririka usoni mwa Amy lakini Ano anabaki mkavu bila kuyumba. Anaonekana kuwa na hasira kidogo.
Kisha wote watatu wanaketi kuzungumza faraghani. Baadaye, mapacha hao wanasema mama yao alieleza kuwa alikuwa mgonjwa baada ya kujifungua na akazimia.
Alipozinduka, wafanyakazi wa hospitali walimwambia muda mfupi baada ya watoto hao kuzaliwa, walifariki. Alisema kukutana na Amy na Ano kumeyafanya maisha yake kuwa na maana mpya. Ingawa hawako karibu, bado wanawasiliana.
Kundi la Facebook
Kundi la Facebook ambalo mapacha walilitumia, Vedzeb, linamaanisha “natafuta” kwa Kijojia. Lina machapisho mengi kutoka kwa akina mama ambao wanasema wafanyakazi wa hospitali waliwaambia watoto wao wamekufa, lakini baadaye waligundua vifo hivyo havikurekodiwa na watoto wao wanaweza kuwa hai.
Machapisho mengine ni kutoka kwa watoto kama Amy na Ano, wanaotafuta wazazi wao waliowazaa. Kikundi hiki kina zaidi ya wanachama 230,000.
Kilianzishwa na mwandishi wa habari Tamuna Museridze 2021 baada ya kugundua kuwa aliasiliwa. Alipata cheti chake cha kuzaliwa kikiwa na maelezo yasiyo sahihi alipokuwa akisafisha nyumba ya marehemu mamake.
Alianzisha kikundi kutafuta familia yake mwenyewe, lakini kikundi hicho kimeishia kufichua kashfa ya ulanguzi wa watoto iliyoathiri maelfu ya watu, kwa miongo kadhaa.
Amesaidia kuunganisha mamia ya familia, lakini bado hajaipata familia yake. Tamuna aligundua biashara ya kuuza watoto ililienea Georgia kutoka mapema miaka ya 1970 hadi 2006.
Anaamini iliendeshwa na wahalifu na ilihusisha watu kutoka sehemu zote za jamii; madereva wa teksi hadi watu wa juu serikalini. Maafisa mafisadi walighushi hati zinazohitajika kwa kuasiliwa kinyume cha sheria.
“Inakadiriwa watoto wapatao 100,000 waliibiwa,” anasema.
Tamuna anaeleza alihesabu idadi hii kwa kuhesabu idadi ya watu ambao wamewasiliana naye na kuangalia mwaka wa watoto kupotea. Ingawa ni vigumu kuthibitisha idadi kamili.
Tamuna anasema wazazi wengi walimwambia walipoomba kuona miili ya watoto wao waliokufa waliambiwa tayari wamezikwa katika uwanja wa hospitali.
Katika visa vingine wazazi wangeonyeshwa watoto wachanga waliokufa ambao walikuwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Tamuna anasema ilikuwa ghali kununua mtoto, n idola za kimarekani 1,400 kwa msichana na dola za kimarekani 1,500 kwa mvulana. Aligundua kuwa watoto wengine waliishi na familia za kigeni nchini Marekani, Canada, Ulaya, Urusi na Ukraine.
Mwaka 2006 Georgia ilibadilisha sheria yake ya kuasili na kuimarisha sheria za kupambana na biashara haramu, na kufanya kuasili kinyume cha sheria kuwa kugumu.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!