Mauaji ya kiongozi wa Hamas Beirut yazidisha mashaka ya vita

Mauaji ya kiongozi wa Hamas Beirut yazidisha mashaka ya vita

Jeshi la Israel limesema limejiandaa kwa hali yoyote baada ya shambulio mjini Beirut, lililomuuwa naibu kiongozi wa Hamas, na kuchochea hofu ya vita katika Ukanda wa Gaza kugeuka mzozo wa kikanda.

Arouri mwenya umri wa miaka 57 ndiye afisa wa kwanza wa ngazi ya juu wa Hamas kuuawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi makubwa ya angani na ardhini dhidi ya kundi hilo karibu miezi mitatu iliyopita, kufuatia uvamizi wa kushtukiza na mashambulizi dhidi ya miji ya Israel.

Israel haijathibitisha wala kukanusha kufanya mauaji ya Arouri, lakini msemaji wa jeshi lake Daniel Hagari alisema vikosi vya Israel vilikuwa katola hali ya juu ya utayari na vimejindaa kwa hali yoyote.

Israel ilimtuhumu Arouri kwa muda mrefu kuhusika na mashambulizi ya mauaji dhidi ya raia wake, lakini afisa wa Hamas amesema alikuwa muhimu sana katika majadiliano yaliofanywa na Qatar na Misri juu ya matokeo ya vita vya Gaza, na kuachiwa kwa mateka wa Israel walioshikiliwa na Hamas.

Nasser Kanaani, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa Hamas na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, amesema mauaji ya Arouri yatachochea zaidi hamasa ya upinzani na kuongeza motisha katika mapambano dhidi ya wakaliaji wa Kizayuni, siyo tu katika maeneo ya Wapalestina, bali katika kanda nzima na miongoni mwa wapiganiaji wa uhuru kote duniani.

Watu wakiwa wamekusanyika nje ya jengo lililoharibiwa kufuatia mlipuko mkubwa katika kitongoji cha Beirut kusini cha Dahiyeh, Lebanon, Jumanne, Januari 2, 2024.Picha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

UN yaelezea wasiwasi, yaomba kujizuwia

Akizungumza mjini New York jana baada ya mauaji hayo kuripotiwa, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Florencia Soto Nino, aliyataja mauaji hayo kuwa kosa la kimahesabu linalosababisha wasiwasi mkubwa, na linalotilia mkazo kile ambacho Katibu Mkuu Antonio Guterres amekisema juu ya hatari ya kusambaa kwa mzozo huo katika kanda pana, na kutoa wito wa kujizuia.

“Kwa hiyo tunatoa wito tena kwa wanachama wote wa jumuiya ya kimataifa kufanya kila wawezalo ili kuzuia kuongezeka kwa mzozo huko. Kwa sababu ya mvutano unaozidi na kudorora kwa hali katika kanda, tunatoa wito kwa pande zote kujizuilia. Hatutaki kukurupuka kokote, vitendo vyovyote vya kukurupuka ambavyo vinaweza kusababisha vurugu zaidi,” alisema Soto Nino.

Mamia ya Wapalestina waliandamana mjini Ramallah na miji mingine katika Ukingo wa Magharibi kulaani mauaji ya Arouri, huku wakipaza sauti za “Kisasi, kisasi, Qassam!” wakimaanisha tawi la kijeshi la kundi la Hamas, ambalo linapambana na vikosi vya Israel Gaza.

Serikali ya Lebanon yazungumza na Hezbollah kuzuwia kuongezeka

Hofu imetawala juu ya hatua gani zitachukuliwa na kundi la Hezbollah, mshirika mkubwa wa Hamas na ambalo kiongozi wake Sayyed Hassan Nassrallah aliweka wazi kwamba hatua yoyote ya Israel kuwalenga viongozi wa Hamas walioko nchini Lebanon itajibiwa vikali.

Serikali ya Lebanon imesema ilikuwa katika mazungumzo na vuguvugu la Hezbollah kuzuwia kuongezeka kwa mzozo na Israel. Kaimu waziri wa mambo ya nje Abdallah Bou Habib, alikiambia kituo cha BBC 4 cha nchini Uingereza Jumanne usiku, kwamba serikali yake ilikuwa inazungumza na Hezobollah kuwashawishi kutojibu mauaji hayo.

“Tuna wasiwasi sana, [Walebanon] hawataki kuingizwa katika hilo, hata Hezbollah haitaki kuingizwa kwenye vita vya kikanda,” alinukuliwa akisema.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon ilianza “kutayarisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi wa Israel, kwa kuzingatia maagizo ya Waziri Mkuu wa muda Najib Mikati,” Shirika la Habari la Taifa linaloendeshwa na serikali lilisema.

Kundi jengine la Wahouthi nchini Yemen, ambalo limekuwa likizishambulia meli za kibiashara katika bahari ya Shamu kushinikiza Israel kuacha kuishambulia Gaza, limesema litazidisha mashambulizi yake na kutishia kuzilenga pia meli za kivita za Marekani ikiwa lenyewe litalengwa.

Jumla ya Wapalestina 22,313 wameuawa na 57,296 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, imesema wizara ya afya ya Gaza katika taarifa siku ya Jumatano.

Takribani Wapalestina 128 wameuawa na 261 kujeruhiwa katika muda wa masaa 24, iliongeza wizara hiyo. Ujerumani, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa mengine yanaiorodhesha Hama kama kundi la kigaidi.

Chanzo: Mashirika

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!