Mtoto alivyoishi ICU siku 60 baada ya kuugua degedege
Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Sh10.1 milioni kugharamia dawa, vifaatiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU hadi akapona.
Dar es Salaam. Mtoto mwenye umri wa miezi minne amekaa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 60 akitibiwa tatizo la maambukizi kwenye ubongo, yaliyotokana na ugonjwa wa degedege.
Mtoto huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati, Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, ametumia Sh10.1 milioni katika gharama za matibabu kwa siku zote alizopokea matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa hospitali hiyo, mama wa mtoto huyo, Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika hospitalini hapo Novemba 11 mwaka jana.
Kabla ya hapo, alikuwa amekaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni akimuuguza mwanaye aliyepatwa na degedege.
Daktari bingwa wa ganzi na wagonjwa mahututi, ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Huduma za Uangalizi maalumu katika hospitali hiyo, Venance Misago amesema moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla mara nne ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.
“Aligundulika kuwa na maambukizi kwenye ubongo, hali iliyokuwa inasababisha apoteze fahamu mara kwa mara,” ameeleza Dk Misago.
Amesema kwa kawaida mgonjwa hukaa ICU siku tatu hadi 14, lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa kiasi cha kusababisha presha kushuka na kusababisha moyo kusimama mara kwa mara.
Akizungumzia ugonjwa wa degedege, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Julieth Kabengula amesema ni ugonjwa ambao unawapata watu wa rika zote japokuwa huwapata zaidi watoto.
Amesema degedege huwa haina dalili, hivyo ni muhimu kuangalia mabadiliko ya mtoto ili kubaini mapema kama ana tatizo hilo.
“Mtoto huyu alianza na mafua, baadaye akaanza kushindwa kunyonya, homa inapanda akapata degedege, ambayo ilisababisha maambukizi kwenye ubongo,” amesema Dk Julieth.
Amesema mtoto anapokuwa na mabadiliko yoyote ni vema kumuwahisha kituo cha kutoa matibabu, maana wakati mwingine huhitajika matibabu ya sindano na haziwezi kupatikana nyumbani.
Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hamis Shaban amesema degedege inaweza kusababisha athari kama isipotibiwa mapema.
“Degedege inaweza kuleta athari nyingine kama ulemavu, wendawazimu, upofu, kutosikia, kulemaza mikono, miguu na mtindio wa ubongo,” amesema.
Kwa mujibu wa Awadhi Mohamed, mkurugenzi msaidizi huduma za ustawi wa jamii, Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Sh10.1 milioni kugharamia dawa, vifaatiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.
Amesema kupona kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya afya nchini, hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za wagonjwa mahututi.
Mama wa mtoto huyo amesema hali hiyo haikuwa rahisi kwake, hivyo anamshukuru Mungu, madaktari na wauguzi waliomhudumia mwanaye.
“Watu walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki peke yake,” amesema Janeth na kuongeza:
“Nilipitia wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu, nawashukuru madaktari na wauguzi kwa kumpambania.”
Mwaka 2020, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa na wodi ya wagonjwa mahututi yenye vitanda sita pekee, lakini kupitia maboresho yaliyofanyika kwa sasa ina wodi mbili za wagonjwa mahututi zenye vitanda 22.
Dk Misago amesema vitanda hivyo vina mashine za kusafisha mfumo wa hewa, mashine za kusaidia kupumua, mashine za kusaidia moyo, figo na kuzuia damu kuganda pamoja na mashine za uangalizi wa mwenendo wa matibabu ya mgonjwa.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!