Mwaka 2023 ulikuwa mwaka wa machungu mengi,wenye kiwango cha juu cha joto,ongezeko la umaskini na njaa, Vita kuongezeka
Heri ya mwaka mpya 2024 na uwe wa matumaini na ustawi – Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefunga mwaka huu wa 2023 na kukaribisha mwaka mpya wa 2024 akisihi kila mkazi wa dunia aazimie kuufanya mwaka huo wa 2024 kuwa mwaka wa kujenga kuaminiana na matumaini kwenye kila ambacho jamii inaweza kufanikisha pamoja.
Machungu yalitawala 2023
Katika ujumbe wake alioutoa Alhamisi Desemba 28, Katibu Mkuu amesema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu mwaka huu wa 2023 umekuwa mwaka wa machungu mengi, ghasia, na zahma ya tabianchi.
“Ubinadamu uko kwenye maumivu, sayari yetu iko hatarini, Mwaka 2023 umekuwa mwaka wenye kiwango cha juu cha joto, watu wanasiginwa na ongezeko la umaskini na njaa, Vita vinaongezeka kwa idadi na ukubwa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa cha kustaajabisha zaidi kuaminiana nako kunazidi kupungua.
Kunyoosheana vidole na silaha si jawabu
Halikadhalika ameonya kuwa “kunyoosheana vidole na kuelekezeana silaha hakutufikishi kokote. Ubinadamu ni thabiti zaidi pindi tunaposimama pamoja.”
Ni kwa kutambua hilo ndipo Katibu Mkuu Guterres anataka kuona mwaka wa 2024 unakuwa mwaka wa kujenga upya kuaminiana na kurejesha matumaini.
Ili hilo lifanyike, Katibu Mkuu anasema “ni lazima tushikamane pamoja kwenye mgawanyiko kwa ajili ya majawabu ya pamoja.”
Mfumo wa fedha duniani uhudumie wote kwa usawa
Majawabu hayo ya pamoja ni “kwa ajili ya hatua kwa tabianchi. Kwa ajili ya fursa za kiuchumi na mfumo wa fedha wa kimataifa unaohudumia watu wote kwa usawa.”
Katibu Mkuu mara kwa mara amekuwa akitaka mfumo wa fedha duniani ufanyiwe marekebisho ili uweze kuhudumia nchi zote na watu wote kwa usawa bila kujali tajiri au maskini.
Amekuwa akitolea mfano wakati wa janga la COVID-19 ambako mashirika ya fecha duniani yalitumia vigezo vya kupatia nchi misaada ya kifedha, vigezo ambavyo vilikuwa ‘mwiba’ kwa nchi maskini hata zikashindwa kuweka mifumo ya kujengea mnepo wananchi wake dhidi ya athari hasi za mlipuko wa COVID-19.
Mwaka 2024 uwe wa mshikamano, Akili Mnemba inufaishe wote
Ametaka pia mwaka 2024 utumike kujenga zaidi mshikamano wa pamoja “dhidi ya ubaguzi na chuki inayotia sumu uhusiano kati ya nchi na jamii.”
Halikadhalika kuhakikisha teknolojia kama vile Akili Mnemba, au AI zina manufaa badala ya kuleta zahma duniani.
Umoja wa Mataifa uko kidete
Guterres amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kuhamasisha dunia yenye amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu, kama ilivyowekwa bayana kwenye Chata ya kuanzisha chombo hicho chenye wanachama 193 mwaka 1945 huko San Francisco Marekani.
Ametamatisha ujumbe wake akisema, “nakutakieni Mwaka Mpya wenye furaha na amani.”
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!