Nilianza kupata maumivu baadaye, nikinywa vitu vya baridi meno yanapata ganzi,madhara ya 'ku-bleach' meno yako
Nilianza kupata maumivu baadaye, nikinywa vitu vya baridi meno yanapata ganzi,madhara ya ‘ku-bleach’ meno yako,
Lipo wimbi la kina dada, hasa wanaotarajiwa kuwa mabibi harusi kwenda hospitali kusafisha meno maarufu kama ku-bleach, jambo ambalo linaelezwa na wataalamu kuwa lina madhara baadaye kwenye safu za meno yao.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya watu hasa wanawake, wamekuwa na utaratibu huo, wengi wao wakifanya hivyo kwa ajili ya urembo.
“Nilianza kwenda kusafisha meno mwaka jana, baada ya kuona siumwi na kadi yangu ya bima inakatwa pesa kila mwaka bila huduma,” alisema Magreth Joseph mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam.
Alisema aliona huduma hiyo kwenye mitadao na kwenda kwenye moja ya hospitali binafsi za Manispaa ya Kinondoni kuuliza taratibu, hivi sasa nimekuwa mteja wao mzuri wa kusafisha meno.
“Sijapata madhara yoyote tangu nimeanza, meno yangu sasa ni meupe kama tui la nazi, nayafurahia hata nikiwa mbele za watu muda wote natabasamu,” amesema Magreth.
Mtumiani mwingine wa huduma hiyo ni Wema Elias ambaye amesema alikwenda kusafisha meno yake siku tatu kabla ya ndoa yake, kwa kuwa alitaka kuwa na muonekano bora zaidi kwenye harusi yake.
“Niliona mtandaoni mtu mmoja alikuwa na meno meupe, nikapenda nikaenda kufanya hivyo kwa mara ya kwanza siku tatu kabla ya harusi yangu. Sijapata madhara yoyote labda kwa baadaye, lakini sasa naifurahia hii huduma” alisema.
Lakini kwa Anthony Lucas, mbaye mwaka 2018 ‘alibleach’ meno yene, anasema mwanzoni alifurahia kutokana na muonekano lakini sasa mambo yamebadilika.
“Nilianza kupata maumivu baadaye, nikinywa vitu vya baridi meno yanapata ganzi. Nimeacha kabisa kwa sasa, nasafisha kinywa kwa kupiga mswaki tu,” amesema.
Faida, hasara
Daktari wa kinywa na meno wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Glory Leo anasema kila kitu kina faida na hasara zake, ikiwemo huduma hiyo ya ‘ku-bleach’ meno.
“Kuna njia mbili za kusafisha meno, kama ni mgonjwa tunamfanyia check-up (uchunguzi) kuona kama kweli anahitaji huduma hiyo.
Anasema hiyo ni kwa wale wenye ugaga, wanakuwa na uchafu uliogandia kwenye meno ambao hauwezi kutoka kwa kupiga mswaki.
“Hospitali kuna kifaa cha kubandua huo ugaga, mara nyingi wenye ugaga ni watu wanaovuta sigara au kula sana vitu vya rangi au wanaokula mirungi.
“Mwenye ugaga, kwanza fizi zake zinabana na kukosa hewa, zinavimba na kusababisha meno kutingishika.
“Anapokula anatoa damu, kinywa kinatoa harufu na wakati mwingine usaha. Anaweza kuwa na meno ambayo hayajatoboka, lakini inatokea tu jino lake likadondoka, pia yanajitawanya na kumsababishia mwanya, hivyo hawa ndiyo wanaosafisha meno.”
Kwenye ku-bleach ili meno yawe meupe (dental whitening) ni jambo jingine na lina faida na hasara zake.
“Wanaopenda ku-bleach sana ni kina dada, mara nyingi huwa tunawashauri kwanza namna ya kufanya meno kuwa meupe bila ku-bleach, maana kwenye meno kuna leyer (safu) ambayo unaposafisha hospitali unaitoa.
“Ile leyer unapoitoa ndipo kuna watu utasikia akila kitu cha baridi anapata ganzi ya meno na madhara mengine kama hayo,” amesema daktari huyo.
Njia rafiki kusafisha meno
Dk Glory anasema njia nzuri ya kusafisha meno, kama huna tatizo la ugaga, ni kutumia mswaki unaofikia kirahisi sehemu zote za kinywa chako.
“Uwe ni saizi yako, siyo mkubwa wala mdogo sana na usiwe mgumu sana au mlaini sana, uwe ni wa saizi ya kati unaotosha kwenye kinywa chako.
“Pia tunashauri kupiga mswaki mara mbili kwa siku, utumie dawa yenye flouride, pia ulaji wako wa sukari unaweza kuwa chanzo cha meno kuharibika.
“Kubwa zaidi watu wengi hawana utaratibu wa kufanya check-up ya meno, waanze kufanya mara mbili kwa mwaka hii itawasaidia hata kujua mabadiliko gani wanayo kwenye meno.
Alisema, mtu anapaswa kutumia mswaki mmoja si zaidi ya miezi mitatu, unapoona unasugua meno na brushi za mswaki zinadondokea mdomoni huo haufai tena.
“Hapa kwenye miswaki, wengi wanataka kufanya biashara, unapokwenda kununua iwe kama maji, yapo mengi lakini unaangalia ni yapi mazuri, hata miswaki, ununue ambayo brashi zake zimesimama na zisiwe ngumu wala laini, ziwe katikati na ukiona imeanza kulala, hata kama miezi mitatu haijafika ubadilishe,” alieleza.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!