Onyo kuhusu tsunami limetolewa Japani baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea

Onyo kuhusu tsunami limetolewa Japani baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea.

Serikali ya Japan imetoa onyo kubwa la Tsunami baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.6 kupiga eneo la pwani la Noto huko Ishikawa, eneo la kati,

Japan pia iliwataka wakaazi “kuhama mara moja” huku kukiwa na onyo la mawimbi ya juu kama 5m.

Mamlaka pia ilitoa maonyo ya tsunami kwa wilaya za jirani za Niigata na Toyama, ambapo walisema mawimbi yanaweza kufikia mita 3.

Televisheni ya umma ilimulika “EVACUATE” kwa herufi kubwa, na kuwataka wakazi kukimbilia maeneo ya juu licha ya baridi.

Mtangazaji wa NHK aliwahimiza watazamaji walioathiriwa: “Tunatambua nyumba yako, mali zako zote ni za thamani kwako, lakini maisha yako ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Kimbilia hadi mahali pa juu zaidi iwezekanavyo.”

Msururu wa matetemeko ya ardhi yalikumba eneo la Noto mchana, kuanzia na tetemeko la kipimo cha 5.7 saa 16:06 saa za huko (07:06 GMT), Shirika la Hali ya Hewa la Japan lilisema. Hili lilifuatiwa na tetemeko hilo la ukubwa wa 7.6 na mitetemeko mingine mitano ndani ya saa moja.

Msemaji wa serikali ya Japan, Yoshimasa Hayashi, amewaonya wakazi kujiandaa kwa tetemeko zaidi.

Kampuni kubwa zaidi ya nishati ya nyuklia nchini humo, Kansai Electric, ilisema “hakujakuwa na hali isiyo ya kawaida” katika vinu vya nyuklia katika eneo lililoathiriwa.

Shirika la hali ya hewa la Korea Kusini limeonya kwamba mawimbi ya tsunami hadi mita 0.3 yanaweza kukumba pwani ya mashariki mwa nchi hiyo kati ya 18:29 hadi 19:17 saa za ndani.

Urusi imetoa tahadhari ya kutokea kwa tsunami katika miji ya bandari ya mashariki ya mbali ya Vladivostok na Nakhodka, shirika lake la habari la serikali TASS liliripoti.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!