SIMAMIENI USAFI KATIKA MAENEO YENU (KIPINDUPINDU KINALETWA NA UCHAFU)
NA: WAF, Mwanza
Watendaji wa kata na mwenyeviti wa mitaa wametakiwa kusimamia usafi katika maeneo yao ili kuendelea kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga mkuu wa serikali Prof Tumaini Nagu Leo Januari 25, 2024 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwenye ofisi za mkuu wa wilaya Mhe. Amina Makilagi wakati wa kikao na watendaji wa Kata juu ya kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu katika Jiji hilo.
Prof. Nagu amewaomba watendaji kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Usafi wa mazingira katika makazi ya wananchi kwa kusimamia kwani ugonjwa huu unasababishwa na Uchafu.
“Kipindupindu kinaletwa na uchafu, hivyo maeneo yetu lazima tuyalinde kwa kufanya usafi bila ya usafi ugonjwa huu utawaathiri wengi. Njia pekee ya kuudhibiti ni kuwa wasafi katika maeneo yetu”. Amesema Prof. Nagu
Sambamba na hilo Prof. Nagu amesisitiza unawaji wa mikono kwa kutumia maji safi na salama pamoja na kunywa maji yaliyochemshwa au kutibiwa kwa dawa ambazo zinatolewa bure na serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ameelezea mikakati ya kuhakikisha ugonjwa wa Kipindupindu unadhibitiwa katika Halmashauri yake ikiwa ni Pamoja na kuendelea kuwatumia watendaji na mwenyeviti katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu.
Hali ya ugonjwa wa Kipindupindu imeendelea kuimarika katika mkoa wa Mwanza kutokana na juhudi za serikali katika kuwekeza nguvu kwenye kuudhibiti ugonjwa huu kwa kutoa Vifaa tiba, Vifaa kinga na dawa.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!