Una sidiria nyeusi, fahamu siri ya wengi kuzitumia

Una sidiria nyeusi, fahamu siri ya wengi kuzitumia

Muktasari:

Daktari anasema kuvaa nguo ya ndani kwa muda mrefu kufanya bakteria wakusanyike kwenye nguo hiyo.

Dar es Salaam. Hii haiwahusu wanawake wa hali ya chini pekee, ipo hata kwa wenye kipato cha juu wanaoweza kununua sidiria kutoka kwa wabunifu mitindo maarufu duniani.

 Sidiria iwe ya rangi yoyote, uwe nazo mbili, tatu au hata begi zima, bado wengi hujikuta wakirudia kuvaa nyeusi.

Hayo yamesemwa jana Jumamosi, Januari 12, 2023 na wanawake mbalimbali waliohojiwa na Mwananchi Digital wakieleza sababu za wao kupenda kuvaa sidiria fulani zaidi kuliko nyingine, huku wengine wakikiri hata kukawia kuzifua.

Licha ya tabia hiyo kwa wanawake, Dk Diva James kutoka hospitali ya mkoa wa Dodoma amesema kuvaa nguo ya ndani kwa muda mrefu kufanya bakteria wakusanyike kwenye nguo hiyo.

“Hii husababisha sidiria kuanza kutoa harufu na endapo akiwa na michubuko midogomidogo inaweza kusababisha bakteria kuingia mwilini na kusababisha maambukizi,” amesema.

Mkazi wa Dodoma, Yusta Mbunda amesema ana sidiria nyingi japokuwa zipo mbili anazozipenda zaidi:

“Nyeusi na khaki yaani hizi mbili kila wiki nazifua. Sijui kwa nini nikizivaa nahisi najisikia vizuri, hazinibani wala hazikai vibaya tofauti na hizi nyingine nilizinunua ghali ila hazinikai vizuri.”

Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Neema maarufu Mama Faiza amesema ana sidiria tano lakini amekuwa akiipenda nyeusi.

“Ninayo hiyo ni bandika bandua, nyeusi hiyo hata kama mvua imenyesha naisubiria ikauke pale juu ya kamba naichukua naitundika naondoka,” anasema.

“Kwa sababu sidiria nyeusi inaficha uchafu, sasa mimi utanivalisha sidiria nyeupe wiki moja au mbili nasimama muda wote sipati muda wa kufua si nitatia aibu,” amesema.

Neema amesema balaa huibuka siku anapoamua kuifua sidiria hiyo: “Unakuta maji meusi hatari mpaka unajiuliza hii sidiria nilivaa mimi au alivaa mwenzangu, zingine ninazo; ya kijivu, nyeupe na nyekundu lakini hii nyeusi inakoma.”

Akieleza sababu za kuipenda zaidi sidiria hiyo, Neema amesema akiivaa humpa mwonekano mzuri tofauti na zingine ambazo humbana na kujihisi hayupo huru.

“Hii nyeusi naweza kuivaa mpaka wiki mbili,” amesema.

Mkazi wa Ilala, Chiku Juma amesema anazo sidiria tano ila anapenda zaidi nyeusi ndiyo huivaa wakati wote.

“Nyeupe siipendi ila hii nyeusi hata kama sijaoga na nataka kutoka nje naivaa. Pia inanipa uhuru wa kuirudia na kusema ukweli naweza kukaa hata wiki sijaifua,” anasema.

Mwajuma Rajab, mkazi wa Tabata, amesema yeye anapenda sidiria nyeusi ingawa anazo nyingi lakini hiyo anahisi inamfaa zaidi.

“Nyeusi. Ninazo nyingi lakini hiyo ndiyo naivaa wakati wote, sababu naiona ndiyo inanifaa zaidi inanikaa vizuri na ninavalia nguo yoyote, hii niliinunua bei rahisi, yaani hata nikifua nguo zangu zote weekend siku naenda kazini Jumatatu nitatungua ileile ninayoipenda,” amesema.

Zainabu Ally, mkazi wa Vingunguti maarufu Zai Kijiwe Nongwa amesema suala la kurudia sidiria, kuvaa kwa muda mrefu haliwahusu kinamama wa Uswahilini pekee.

“Nina mashoga zangu wanakaa huko Mbezi Beach wanatoka matawi ya juu, unakutana naye anakwambia anapenda kuvaa moja au mbili hizohizo anacheza nazo,” anasema.

“Mwingine anakwambia ninayo rangi ya ugoro ninaipenda sana maana inaficha mengi, kikubwa nilichobaini kila mwanamke ana sidiria yake inayomtosha ni ngumu kumshauri aachane na anayoipenda, waume wanatununulia tunaziacha kabatini unavaa ileile,” amesema.

Akielezea Uswahilini, Zai amesema wanawake wa huko wananunua zaidi sidiria za rangi ya ugoro, nyeusi au chuichui na wafanyabiashara wanajua hawauzi nyeupe, pinki wala za rangi ya maziwa.

“Kinamama wa Uswahilini huku wanavaa sidiria mpaka zinafanana nao mwili, na wanaume wanasema wanawanunulia wake zao lakini kesho anamkuta kaivaa ileile aliyomkataza, sijajua kwanini wanawake tupo hivi, wengine wanavaa mpaka zinawachimba kwenye mabega na wengine mpaka vile vichuma vinavyobeba matiti vinakatika,” amesema. Via:Mwananchi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!