Waandishi wachomwa visu wakifuatilia habari za shisha

Waandishi wachomwa visu wakifuatilia habari za shisha

Nairobi. Waandishi wa habari wawili kutoka Kenya wanadaiwa kupigwa, kuchomwa visu na walinzi wa baa, wakiwa klabu ya usiku wakifuatilia habari kuhusu matumizi ya shisha. Tovuti za Tuko na Nation zimeripoti.

Inaelezwa wanahabari hao walikuwa na askari polisi pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Kupambana na Matumizi Mabaya ya Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada) katika msako wa matumizi ya shisha yaliyopigwa marufuku nchini humo.

Tukio hilo limetokea Ijumaa ya Januari 5, 2024 katika baa ya Kettle House huko Lavington jijini Nairobi ambapo pia ofisa wa Nacada na baadhi ya askari polisi walijeruhiwa.

Tovuti ya Nation imesema baada ya kuwaona waandishi wa habari watu hao wakiwa wamevalia suti nyeusi na tai nyekundu waliwapiga na kuwanyang’anya kwa nguvu vifaa vyao vya kazi.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni mpigapicha wa Nation Media, Boniface Bogita, ambaye alichomwa kisu mara mbili ubavuni. Jane Kibira, mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Kenya pia alidungwa kisu mgongoni.

Pia, mpiga picha wa Standard Media Group, Boniface Okendo na Francis Odee walipigwa na kamera zao kuchukuliwa.

Baadaye polisi walidhibiti hali hiyo na kuwakamata washambuliaji waliokuwa wamekimbia kubadilisha nguo na kujificha kwenye vyoo vya baa hiyo, ili kukwepa kukamatwa.

Nacada ilikuwa inaendesha msako mkali wa kuzuia uvutaji wa shisha kufuatia kuharamishwa nchini humo tangu 2017, ikiwa ni pamoja na kuitangaza, kuikuza, kuisambaza na kuhimiza au kuwezesha matumizi yake nchini Kenya.

Muungano wa Wanahabari wa Kenya (KUJ) umejitokeza kulaani tukio hilo. Katika taarifa yake ya jana Jumamosi, Januari 6, 2024, Katibu Mkuu wa KUJ, Erick Oduor ameomba wahusika wachukuliwe hatua.

Ametoa wito kwa polisi kuhakikisha watuhumiwa wanakabiliana na mkono wa sheria na kumtaka mmiliki wa jumba hilo la burudani kuwajibika kwa uharibifu uliotokea.

Hadi sasa watu 21 wamekamatwa na wanasubiri kufikishwa mahakamani.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!