Watatu waliogundulika na kipindupindu waruhusiwa

Watatu waliogundulika na kipindupindu waruhusiwa

Watu watatu kati ya watano waliobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu katika kata ya Kagongo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri hiyo, Dk. Shani Josephat, amesema kuwa wawili waliogundulika na ugonjwa huo wanaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Mwendakulima.

Dk. Josephat alisema Januari 2, mwaka huu, kuliripotiwa watu watano kuwa na dalili za ugonjwa wa kipindupindu hali iliyowafanya kuchukua sampuli zao na kuzipima katika maabara hospitalini hapo, huku zaidi ya 500 wakiendelea kuwa karantini.

“Tunaendelea na kukabiliana na tatizo hili kwa kuzitembelea kaya na kuzipatia elimu ya namna ya kujikinga kwa kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka, kwani ugonjwa huu ni hatari na unaua,” alisema.

Alisema watu wanaobainika kuwa na ugonjwa huo wanapatiwa huduma katika Kituo cha Afya Mwendakulima na tayari wameelekeza nguvu katika kata hiyo ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae.

“Timu yetu ya watalaamu wa afya imeweka kambi katika kata hiyo kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kuzuia ugonjwa huo usiendelee kuenea zaidi kwenye kata nyingine.

“Mpaka sasa visa vyote vya ugonjwa huu viko ndani ya kata hii pekee na wale wanakaya walioruhusiwa tunawafuatilia kwa ukaribu ili wasije kupata ugonjwa huo kwa mara nyingine,”alisema Dk. Josephat.

Alisema wahisiwa wote waliopokelewa katika kituo hicho cha afya hakuna hata mmoja aliyepoteza maisha, wametibiwa na wengine wameruhusiwa. Alisema mpaka sasa katika kituo cha tiba na mafunzo kuna wagonjwa 13 ambao pia, afya zao zinaendelea kuimarika.

Mkazi wa Kagongwa, Kevin Godgrey, alishauri kuzifikia kata nyingine na kuzipatia elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, kwani baadhi yao wamekuwa wakifika katika kata hiyo kupata mahitaji ya familia.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!