Watu 12 wathibitika kuwa na kipindupindu mmoja afariki dunia Geita

Watu 12 wathibitika kuwa na kipindupindu mmoja afariki dunia Geita

Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao cha mikakati ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Kipindupindu.

Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaendelea kuenea mikoa ya Kanda ya Ziwa baada ya mikoa ya Mwanza na Kagera kukumbwa na ugonjwa huo sasa Geita nayo yatangaza.

Watu 12 wamethibitika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu Mkoani Geita huku mmoja kati yao mzee mwenye umri wa miaka 99 amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela akiwa kwenye kikao cha mikakati ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Kipindupindu. Picha na Mrisho Sadick

Akitangaza uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa huo Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya msingi cha kuweka mikakati ya kuzuia kusambaa kwa Ugonjwa huo amesema wagonjwa tisa walibainika wilayani Mbogwe na watatu kutoka wilaya ya Chato ambapo wote wametibiwa nakuruhusiwa huku mmoja kati yao mzee mwenye umri wa miaka 99 kutoka wilayani Mbogwe alifariki Dunia wakati akipatiwa matibabu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt  Omari Sukari  amesema  kusambaa kwa mlipuko huo wilayani Mbogwe umetokana na maji ya kisima kukutwa na vimelea ambacho kipo mita chache kutoka kwenye choo.

Omari Sukari Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita akiwa kwenye kikao cha mikakati ya kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Kipindupindu.

Wataalamu kutoka mamlaka za maji mjini Geita ikiwemo GEUWASA na RUWASA wametumia kikao hicho kuishauri juu ya matumizi ya maji ili kuepukana na changamoto ya kukumbwa na ugonjwa huo.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!