Watu watano wabainika kuwa na vimelea vya Ugonjwa wa kipindupindu Kahama Shinyanga
Watu watano wabainika kuwa na vimelea vya Ugonjwa wa kipindupindu Kahama Shinyanga.
Watano wathibitika kuugua, 13 walazwa na 452 waliochangamana na wagonjwa wafuatiliwa na watalaamu wa afya
Shinyanga. Watu watano wamethibitika kuugua ugonjwa wa kipindupindi uliolipuka katika mji mdogo wa Kagonga, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mlipuko wa ugonjwa huo umethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita leo Ijumaa, Januari 5, 2024 katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hadi leo jioni, watu 13 walikuwa wamelazwa kwa matibabu katika kituo cha afya Mwendakulima na wataalamu wa afya wanaendelea kuwafuatilia watu wengine 452 wanaodaiwa kuchangamana na waliothibitika kuugua ugonjwa huo.
“Kituo cha afya Mwendakulima kimetengwa maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wanaothibitika kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu,” amesema DC Mhita.
Amesema tayari Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti ugonjwa huo ulioripotiwa kuibuka wilayani humo tangu Januari 2, 2024 ikiwemo kuwatenga wanaohisiwa kuambukizwa.
“Timu ya wataalamu tayari ipo Mji mdogo wa Kagongwa kutoa elimu kwa umma namna ya kuepuka maambukizi na kuhudumia wagonjwa ambao tayari wameambukizwa,” amesema Mhita.
Kutokana na ugonjwa huo, Serikali imepiga marufuku biashara ya kuuza pombe za kienyeji kwa kufunga vilabu vyote katika mji mdogo wa Kagonga ambako pia mikusanyiko isiyo ya lazima imezuiliwa.
Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk Shani Mdami amesema hadi sasa hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kagongwa, Michael Shija amesema Desemba 25, 2023 kulitokea msiba wa mtoto ambaye kabla ya kufikwa umauti alikuwa akiharisha na kutapika.
“Baba mzazi wa mtoto yule naye alianza kuugua na kufariki dunia baada ya siku mbili. Hali hiyo iliibua taharuki na sisi viongozi kuamua kutoa taarifa kwa mamlaka za juu Januari 2,2024 kwa msaada zaidi ya kiuchunguzi,” amesema Shija.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!