WHO yaitangaza nchi ya Cabo Verde kuwa nchi isiyokuwa na malaria

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeitangaza nchi ya Cabo Verde kuwa nchi isiyokuwa na malaria.

Hongera Cabo Verde kwa kutokomeza malaria.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus (kulia) akiashiria kutokomeza ugonjwa wa malaria huko Cabo Verde akiwa na Waziri Mkuu Ulisses Correia e Silva (katikati) na Waziri wa Afya Filomena Mendes Gonçalves (kushoto).

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeitangaza nchi ya Cabo Verde kuwa nchi isiyokuwa na malaria imetokomeza ugonjwa wa Malaria na kuipatia cheti rasmi.

Sherehe za utoaji cheti hicho zimefanyika jijini GenevaUswisi katika makao Makuu ya WHO ambapo nchi hiyo imekuwa moja kati ya nchi 43 na mamlaka 1 na zilizofanikiwa kutokomeza ugonjwa huo hatari unaosababisha vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka hususan barani Afrika.

Akikabidhi cheti hicho Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameipongeza Cabo Verde kwakufanikiwa katika vita vya kimataifa dhidi ya malaria, na kusema nchi hiyo imetoa matumaini kwamba kwa kutumia zana zilizopo, pamoja na mpya zikiwemo chanjo, dunia inaweza kuthubutu kuwa na ndoto ya ulimwengu usio na malaria.

“Ninaipongeza serikali na watu wa Cabo Verde kwa kujitolea kwao bila kuyumbayumba na ustahimilivu katika safari yao ya kutokomeza malariaa. Cheti cha uthibitisho cha WHO kwa Cabo Verde kuwa haina malaria ni uthibitisho wa nguvu ya upangaji mkakati wa afya ya umma, ushirikiano, na juhudi endelevu za kulinda na kukuza afya. “

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus anakutana na wahudumu wa afya katika Kituo cha Afya cha Santa Cruz huko Cabo Verde.

Safari ya Cabo Verde kutokomeza Malaria 

Kisiwa cha Cabo Verde, chenye muunganiko wa visiwa 10 katika Bahari ya Atlantiki ya Kati, kilikuwa kikikabiliwa na changamoto kubwa za malaria. Kabla ya miaka ya 1950, visiwa vyote viliathiriwa na malaria. Milipuko mikali ilikuwa ikitokea mara kwa mara katika maeneo yenye watu wengi hadi hatua zilizolengwa kumaliza tatizo hilo zilipotekelezwa.

Kupitia matumizi ya unyunyiziaji wa dawa, nchi hiyo ilifanikiwa kutokomeza malaria mara mbili, mwaka 1967 na 1983. Hata hivyo, upungufu wa udhibiti wa vijidudu ulisababisha kurudi kwa ugonjwa huo.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, malaria huko Cabo Verde imekuwa katika visiwa viwili tu: Santiago na Boa Vista, ambavyo sasa vyote havina malaria tangu mwaka 2017.

Safari ya Cabo Verde ya kutokomeza malaria imekuwa ndefu na imepata msukumo, ilijumuishwa katika sera yake ya kitaifa ya afya mwaka 2007. Mpango mkakati wa malaria kutoka mwaka 2009 hadi 2013 uliweka msingi wa mafanikio, ukilenga utambuzi, matibabu ya mapema na ya ufanisi, na kuripoti na kuchunguza wagonjwa wote.

Ili kukomesha wimbi la wagonjwa walioungia nchini humo kutoka bara la Afrika, uchunguzi na matibabu yalitolewa bila malipo kwa wasafiri wa kimataifa na wahamiaji.

Mwaka 2017, nchi hiyo iligeuza mlipuko wa malaria kuwa fursa. Cabo Verde iligundua matatizo na kuyafanyia maboresho, na kusababisha kutokuwepo hata mtu mmoja ndani ya nchi kuugua ugonjwa huo kwa miaka mitatu mfululizo.

Ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na idara mbalimbali za serikali zikiwemo zile za  mazingira, kilimo, uchukuzi, utalii, na mengineyo, ulichukua nafasi muhimu katika mafanikio ya Cabo Verde. Tume iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilikuwa na sehemu muhimu katika kutokomeza malaria.

Waziri Mkuu wa Cabo Verde, Ulisses Correia e Silva katika akiishukuru WHO kwa kuitambua rasmi kama nchi isiyo na malaria aesema “Kuthibitishwa kwetu kuwa nchi isiyo na malaria kuna athari kubwa chanya, na imechukua muda mrefu kufikia hatua hii. Kwa upande wa sura ya nje ya nchi, hili ni jamno nzuri sana, kwa utalii na kwa kila mtu mwingine. Changamoto ambayo Cabo Verde imeshinda katika mfumo wa afya inatambulika”.

Juhudi za ushirikiano na kujitolea kwa mashirika ya kijamii na NGOs nazo zinaonesha umuhimu wa mtazamo kamili kwa afya ya umma.

Cabo Verde imeidhinishwa kuwa nchi isiyo na malaria.

WHO Afrika yaipongeza

Mzigo wa Malaria ndio mkubwa zaidi katika bara la Afrika, ambalo lilichangia takriban asilimia 95 ya wahgonjwa wa malaria duniani na asilimia 96 ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo kwa mujibu wa takwimu wa WHO kwa mwaka 2021.

Cabo Verde ni nchi ya tatu kuthibitishwa kutokomeza malaria katika kanda ya Afrika, ikiungana na Mauritius na Algeria ambazo ziliidhinishwa mwaka wa 1973 na 2019 mtawalia.

“Mafanikio ya Cabo Verde ni mwanga wa matumaini kwa Ukanda wa Afrika na kwingineko.” Amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika akieleza kuwa kufikiwa kwa hatua hii muhimu na Cabo Verde ni mfano wa kutia moyo kwa mataifa mengine kufuata.

“Ushindi huo wa kutokomeza Malaria unaonesha kuwa kwa nia thabiti ya kisiasa, sera madhubuti, ushirikishwaji wa jamii na ushirikiano wa sekta mbalimbali, kutokomeza malaria ni lengo linaloweza kufikiwa.”

Wakati Cabo Verde inaposherehekea mafanikio haya makubwa, jumuiya ya kimataifa nayo imepongeza viongozi wake, wataalamu wa afya, na wananchi kwa kujitolea kwao kutokomeza malaria na kujenga maisha bora ya baadaye kwa wote.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!