Familia ya Mtanzania, Abraham Mgowano aliyefariki Marekani yafunguka
Familia ya Mtanzania, Abraham Mgowano aliyefariki Marekani yafunguka
Dar es Salaam. Familia ya Mtanzania, Abraham Mgowano aliyefariki dunia kwa kuanguka kutoka kwenye boti iliyokodiwa ikifanya safari katika Mto Miami nchini Marekani, imesema taratibu za maziko zinaendelea na mwili wa ndugu yao utarejeshwa nyumbani hivi karibuni.
“Mpango wa kurudisha mwili wake Tanzania unaendelea. Tunatarajia itachukua kati ya siku 10 hadi 15 kuanzia leo,” Alexender Mgowano, kaka wa marehemu, ameiambia Mwananchi Digital.
Amesema mdogo wake huyo amekuwa Marekani tangu Septemba 2010, alipojiunga na Chuo Kikuu cha Stanford na alianza kufanya kazi Google mwaka 2014 baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza.
Mwili wa Mgowano (35), aliyekuwa akifanya kazi kampuni ya Google kama mhandisi wa programu, ulipatikana Jumanne baada ya kupotea tangu alipoanguka kutoka kwenye boti hiyo yenye urefu wa futi 44 Jumamosi ya wiki iliyopita.
Mwili wa Mgowano ulipatikama mwishoni mwa wiki ukielea majini, polisi wamethibitisha.
Kwa mujibu wa maofisa wa Tume ya Kuhifadhi Samaki na Wanyamapori ya Florida (FWC), Mgowano alianguka kutoka kwenye boti yenye urefu wa futi 44 karibu na Hifadhi ya Lummus kwenye kitalu namba 400 katika eneo la kaskazini mwa mto huo.
Tangu siku hiyo, Polisi wa Miami na viongozi wengine walikuwa wakimsaka Mgowano kwa njia ya anga na hata kuwaita wazamiaji kumtafuta majini. Pamoja na jitihada zao, hawakuupata mwili huo hadi walipopigiwa simu juzi kuhusu maiti iliyoonekana ikielea mtoni, hivyo wakaenda kuiopoa.
Hata hivyo, polisi hawakutoa maelezo kuhusu mahali ambapo maiti ya Mgowano ilipatikana au ni nani aliyeipata. Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya tukio hilo iliyotolewa na FWC, watu wengine 12 waliokuwa pamoja na Mgowano waliwaambia wapelelezi wa tukio hilo kwamba walimuona akielea juu ya maji, kisha akazama na hakutokea tena.
Ripoti hiyo inaeleza aliyekuwa akiendesha boti hiyo, Eddy Espinosa Hernandez (39), alikuwa nahodha aliyekodiwa na abiria hao. Hata hivyo, hakupatikana kutoa maelezo yake.
Polisi wamebainisha katika ripoti yao kwamba “hakuonyesha dalili za kuharibika.” Mgowano anatokea Tanzania na alikuwa Marekani akifanya kazi katika kampuni ya Google kama mhandisi wa programu, kama mitandao yake ya kijamii inavyoonyesha.
Mmoja wa marafiki zake wa karibu, Joseph Rwembiza amesema wamempoteza mtu aliyekuwa na mapenzi ya kweli kwa kila mtu na siku zote walikutana kila alipokuja Tanzania kutoka Marekani.
Katika taarifa ya pamoja waliyoitoa kwa Mwananchi Digital, marafiki wa Mgowano walisema, “Abraham alikuwa bora wakati wote. Tunamwita genius (mwenye akili nyingi); alikuwa na moyo mkuu; alitupenda siku zote na kutuonyesha upendo wa kweli. Alituunganisha kila mara alipokuja Tanzania kutembea.”
Rwehumbiza na washiriki wengine wa kikundi hicho kinachoitwa Loyolite, kilichojumuisha wanafunzi wenzake wa zamani waliosoma katika shule ya sekondari ya Loyola, walimaliza kidato cha nne mwaka 2006.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!