Mama ahamia shuleni ili mwanaye mwenye ulemavu aweze kusoma

Mama ahamia shuleni ili mwanaye mwenye ulemavu aweze kusoma

Mbeya. Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, ndivyo ilivyo kwa Itika Mwakamele, mkazi wa Kiwira wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya, aliyebeba jukumu la kumhudumia shuleni mwanaye mwenye ulemavu wa viungo, ili aweze kuendelea na masomo.

 Kutokana na majukumu aliyonayo kwa mwanaye, Itika (46) amehamia shuleni ili awe karibu naye.

Amesema mzazi mwenzake amemkimbia tangu mtoto huyo akiwa na miezi tisa baada ya kubaini ni mlemavu wa viungo.

“Awali nilikuwa nipo sawa na mwenzangu, lakini mtoto alipofikisha miezi tisa na kugundulika ana ulemavu wa viungo aliondoka hadi leo hatujui yupo wapi,” amesema Itika.

Amesema ameomba hifadhi katika Shule ya Sekondari Kiwira anakosoma mwanaye, ili awe karibu naye kwa kumpatia huduma anazohitaji ikiwamo kumpeleka msalani.

Itika amesema mwanaye Samwel Mwakamele (17) amesema Shule ya Msingi Mpandapanda iliyopo Kiwira alikoanza shule ya awali hadi darasa la saba alilohitimu mwaka 2020.

Samwel Mwakamele akiwa amebebwa akirudishwa darasani baada ya kumalizika kwa klabu za masomo.

Amesema walimu walimwambia amuache shuleni na kumpitia baada ya masomo, ili akaendelee na shughuli nyingine kutokana na kutumia muda mwingi kukaa shuleni.

Itika amesema baada ya matokeo ya darasa la saba, Samwel alichaguliwa kwenda kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mwakaleli, akiwa mwanafunzi pekee aliyechaguliwa kujiunga shule ya bweni.

“Niliposikia kachaguliwa Mwakaleli sekondari nikaenda kutembelea shule aliyochaguliwa ndipo nilipokutana na mkuu wa shule, nilimueleza hali halisi ya mtoto kuwa ni wa kusaidiwa kila kitu.

“Mkuu wa shule aliniambia hajawahi kupata mwanafunzi wa aina hiyo, hivyo mazingira yatakuwa magumu kwao,” amesema.

Amesema aliomba iwapo atapa eneo la kuishi shuleni, ili kumhudumia mwanaye lakini ilishindikana.

Amesema alipata ushauri wa kumhamishia shule ya kutwa ili amhudumie, ndipo alipoanza mchakato wa uhamisho kumpeleka Shule ya Sekondari Kiwira.

“Ili kupata uhamisho nilienda na mtoto hadi Halmashauri ya Rungwe, niliwaambia nina hofu ya kuwakwamisha wanafunzi wengine ambao walitakiwa wamuogeshe Samwel, halafu na wao wamalizie,” amesema.

Itika amesema alipoulizwa anaonaje, aliwaambia atafanya kama ilivyokuwa shule ya msingi, angempeleka asubuhi baada ya masomo atamfuata.

Amesema katika kata yao kuna shule mbili za sekondari ambazo zipo karibu na anapoishi za Mpandapanda na Kiwira, hivyo alikubaliwa kumpeleka Kiwira baada ya kuzungumza na mkuu wa shule hiyo aliyeridhia kumpokea.

Hata hivyo, amesema Samwel alipokuwa kidato cha pili mwaka 2022 alianguka akiwa shule na kuvunjika nyonga, hivyo Hospitali ya Wilaya ya Rungwe walisema hawawezi kumtibu akapewa rufaa  Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

“Nilivyoambiwa hawawezi kumtibu na kupewa rufaa sikujua kama tatizo ni kubwa, nilipofika hospitali ya Mbeya nikaambiwa natakiwa kwenda MOI na gharama za matibabu ilikuwa Sh20 milioni,” amesema.

Baada ya kutajiwa gharama, amesema alichanganyikiwa na hali ilizidi kuwa mbaya kwa sababu athari ya nyonga ilisababisha mwanaye kuwa na mguu mmoja mfupi.

Amesema alimweleza mkuu wa shule ambaye pamoja na wanafunzi walichanga fedha ingawa hazikutumia, lakini walionyesha nia ya kumsaidia Samwel.

“Wakati naendelea na mahangaiko alipatikana mfadhili ambaye aliyesema angegharimia matibabu na usafiri. Tulifanikiwa kumtibu, tulikaa MOI miezi minane,” amesema.

Amesema baada ya matibabu, aliomba kwa mkuu wa shule akae hapo, ili kuwa karibu na mwanaye.

Itika amesema jukumu lake ni kumpeleka darasani na kumrudisha kwenye chumba wanachoishi shuleni.

Amesema ilibidi Samwel abaki kidato cha pili. Wenzake walikuwa wameshafanya mitihani ambao kwa sasa wapo kidato cha nne.

Amesema mwanaye alifanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2023 na alipata daraja la pili pointi 19.

Asemavyo Samwel

Samwel amesema changamoto yake ni kuharibika kwa fimbo anayotembelea kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki.

“Sipendi kubebwa, lakini inabidi iwe hivyo kwa sababu hakuna sehemu nzuri ya mimi kupita na wakati mwingine naanguka, hata kifaa ninachotumia  huharibika na ni gharama,” amesema.

Amesema watu wanaombeba wakati mwingine wanachoka, naye hatamani kuhama shule kwa sababu amashazoea mazingira na marafiki wa shuleni hapo.

Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kiwira, Joseph Mwabulesi amesema kutokana na hali ya kijana huyo, msaada unahitajika hususani kwenye miundombinu, kwani wakati mwingine anakosa kuhudhuria klabu za masomo shuleni hapo.

“Tuliomba baadhi ya vijana kumsaidia kumbeba wanapokwenda madarasa mengine kwa ajili ya klabu za masomo, wasipokuwapo ina maana Samwel hawezi kuhudhuria kutokana na hali ya njia za kupita,” amesema.

Amesema endapo Serikali itasaidia kujenga miundombinu kwa ajili ya mwanafunzi huyo itamsaidia mzazi wake kwenda kufanya shughuli zake za kiuchumi, ili kumsaidia kijana wake.

Amesema bado kumekuwa na changamoto kwa Samwel kwenye matumizi ya kompyuta mpakato ambayo alipatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rungwe, baada ya kutembelea shule hiyo na kuona changamoto ya usomaji wake.

“Kutokana na aina yake ya ulemavu Wizara ya Elimu na Baraza la Mitihani (Necta) ilitupa maelekezo namna ya kumtungia mitihani na huwa tunamuingizia kwenye kompyuta,” amesema.

Amesema wakati wa kufanya mtihani Samwel huongezwa dakika 10 zaidi kwa sababu uandikaji wake ni wa taratibu.

Via:Mwananchi

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!