Mlipuko mkubwa wa gesi watokea Kenya na kua watu watatu kisha kujeruhi takriban 300
Mlipuko mkubwa wa gesi watokea Kenya na kua watu watatu kisha kujeruhi takriban 300
Mlipuko mkubwa wa gesi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, umesababisha vifo vya takriban watu watatu na na kuwajeruhi wengine takriban 300.
Lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi lililipuka katika wilaya ya Embakasi mwendo wa 23:30 (20:30 GMT), “na kuwasha moto mkubwa”, msemaji wa serikali alisema.
Nyumba, biashara na magari viliharibiwa huku video ikionyesha moto mkubwa ukiwaka karibu na majengo ya ghorofa.
Hapo awali, serikali ilikuwa imesema mlipuko huo ulitokea katika kiwanda cha gesi. Sababu bado inachunguzwa.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema eneo la mlipuko sasa limezingirwa na kituo cha kuendesha operesheni ya uokoaji kimeanzishwa kusaidia kuratibu shughuli za uokoaji.
“Wakenya wanashauriwa kuepuka eneo lililozingirwa ili kuruhusu shughuli ya uokoaji kutekelezwa [bila] usumbufu ,” aliongeza.
Moto huo unaripotiwa kuenea katika majengo kadhaa ya ghorofa, na kusababisha hofu kwamba idadi ya waliojeruhiwa inaweza kuongezeka zaidi.
Mashahidi waliambia vyombo vya habari kuwa walihisi tetemeko mara baada ya mlipuko huo.
Mmoja wa waliojeruhiwa, Boniface Sifuna, alielezea kilichotokea kwa shirika la habari la Reuters: “Nilichomwa na mtungi wa gesi uliolipuka nilipokuwa nikijaribu kutoroka,” alisema.
“Ililipuka mbele yangu na athari iliniangusha chini na miali ya moto ilinikumba. Nina bahati kwamba nilikuwa na nguvu za kutosha kuondoka.”
Shahidi ambaye jina lake halikutajwa akiongea na gazeti la Nation alizungumzia “milipuko mikubwa, mipira mikubwa ya moto, watu kupiga mayowe na kukimbia kila mahali kwa kuhofia milipuko zaidi”.
Mwandishi wa habari wa Nation anayeishi katika eneo hilo alisema kila mtu alikuwa ameondoka nyumbani kwake baada ya mlipuko huo.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba wafanyakazi wamekuwa “wakipambana na moto huo bila kuchoka”.
Via:Bbc
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!