Nchi zilizo kwenye hatari ya kusambaza Ugonjwa wa kipindupindu kwa Wengine zatajwa

Nchi zilizo kwenye hatari ya kusambaza Ugonjwa wa kipindupindu kwa Wengine zatajwa.

Idadi ya wagonjwa wa kipindipindu hususan Mashariki na kusini mwa Afrika imeongezeka mara mbili mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana ambapo jumla ya wagonjwa 26,000 na vifo 7000 vimeripotiwa katika wiki nne za mwanzo wa mwaka huu kutoka nchi 10 zikiongozwa na Zambia na Zimbabwe.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao huko Geneva Uswisi, Meneja wa operesheni za dharura wa Shirika la Afya Duniani -WHO kanda ya Afrika Dkt. Fiona Baraka amezitaja nchi nyingine kuwa ni “ Msumbiji, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Ethiopia na Nigeria. Hizi ni nchi zilizo kwenye hatari ya kusambaza ugonjwa huu kwa nchi nyingine.”

Miongoni mwa sababu ya idadi hiyo kubwa ya vifo ni unyanyapaa ambapo watu wengi hawaendi vituo vya afya hivyo WHO inashirikiana na nchi husika kutoa elimu kwa umma.

Miradi ya afya Kenya

Nchini Kenya Bodi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID leo limeendelea na ziara yake kukagua faida za miradi bunifu ya kuimarisha sekta ya afya ambayo imeboresha maisha ya maelfu ya wakenya na wakati huo huo kuokoa fedha.

Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa shirika hilo tanzu la lile la Umoja wa Mataifa la afya, WHO akizungumza kutoka Nairobi, Kenya amesema “kwa ushirikiano na Kenya, UNITAID imeanzisha matumizi ya vipimo vya mapema vya Virusi Vya Ukimwi kwa watoto, dawa bora za kupunguza makali ya Ukimwi kwa watoto, dawa rafiki kwa watoto dhidi ya Kifua Kikuu, uchunguzi wa kisasa na tiba dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, chanjo mpya ya Malaria na ufikiaji rahisi wa uchunguzi na tiba dhidi ya COVID-19.”

Via:UN

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!