Rais Samia amjulia hali mama Halima Mdee hospitali

Rais Samia amjulia hali mama Halima Mdee hospitali.

Rais Samia amemtembelea mama mzazi wa mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee aliyelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma.

Ni ziara yenye faraja, hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtembelea mama mzazi wa mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee aliyelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma.

 Alipofika kwenye hospitali hiyo leo Februari mosi, 2024, Rais Samia amemtembelea mama mzazi wa mbunge huyo aliyelazwa hospitalini hapo akisumbuliwa na saratani.

Katika wodi aliyolazwa mama huyo, Rais Samia akiwa ameambata na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu walipokelewa na Halima na mbunge mwenzake, Ester Bulaya.

Kama ilivyo ada mgeni anafika kumtazama mgonjwa, anayemuuguza ndiye anayetoa taarifa ya maendeleo ya mgonjwa hivyo ndivyo alivyofanya Halima akimuelezea Rais Samia hali ya mama yake.

Wakati wote wa mazungumzo wodini hapo, vicheko na tabasamu vilitawala hasa pale mama Halima alipoeleza mapenzi yake kwa Rais Samia.

Hisia hizo zilithibitishwa na Halima mwenyewe aliyeeleza mara kwa mara amekuwa akihojiwa na mama yake kuhusu harakati zake za kisiasa zenye mrengo wa kuisumbua Serikali inayoongozwa na Rais Samia.

“Yaani anakupenda kweli hadi wakati wengine tukiwa wakali kidogo ananiambia sasa nyie mnamsumbua mama yenu, namwambia tuache tu tuko kazini,” amesema Halima.

Kauli hiyo ilimfanya Rais Samia kuangua kicheko na kusema, “Kumbe nina watetezi, hiyo ndiyo bahati yangu wanawake hawana compromise,” amesema.

Baada ya vicheko vya hapa na pale, Rais Samia aliaga familia hiyo na kuendelea na ziara hospitalini hapo na moja kwa moja akaelekea kwenye dawati wanalokaa wauguzi na kupiga nao picha na kuwapa ujumbe wake.

 “Endeleeni kuchapa kazi, kumrudishia mtu uzima wake mna fungu kubwa kwa Mungu, hivyo nawaomba msichoke. Mie najituma sichoki, hivyo nawaomba na nyie msichoke,” amesema Rais Samia.

Via:Mwananchi

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!