Ticker

6/recent/ticker-posts

Saba wapofuka wakitibu ‘red eyes’ kienyeji



Saba wapofuka wakitibu ‘red eyes’ kienyeji.

Takriban watu 7 wapofuka baada ya kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa wa macho. Watu 12,860 wameathirika na ugonjwa wa ‘red eyes’ na wengi wao hawapati matibabu. Serikali yatoa wito wa elimu zaidi kuhusu matumizi sahihi ya tiba.

Unguja. Watu saba wamepofuka macho baada ya matumizi ya dawa za kienyeji kutibu ugonjwa wa macho mekundu (Red eyes) Zanzibar.

Mbali ya hao, zaidi ya watu 12,860 wameugua ugonjwa huo, wengine wakiwa wamepona na baadhi wanaendelea na matibabu.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa huduma za afya msingi ya matibabu ya macho, Dk Rajab Muhammed Hilali kuwa dawa za kienyeji zimewasababishia upofu watu hao.

Amesema miongoni mwa wagonjwa waliopata upofu yupo mtoto wa miaka 11 ambaye jicho lake la kulia limeathirika na walifanya jitihada za kumpeleka Hospitali ya CCBRT lakini ilionekana haliwezi kurejea katika hali ya kawaida.

Dk Rajab amesema watu wengi wanaoenda hospitalini wanakuwa wameshazidiwa baada ya kutumia dawa ambazo si sahihi katika tiba.

“Kwa wagonjwa hao wana jicho ambalo limepata upofu, ukiuliza unaambiwa alikuwa anatumia dawa za kienyeji, chumvi na vitu vingine kwa hiyo vimeleta athari kwenye jicho,” amesema.

Meneja wa kitengo cha elimu ya afya cha Wizara ya Afya, Dk Bakar Hamad Madarawa amesema kuna wagonjwa wengi waliougua ugonjwa wa macho lakini hawajaenda kupata matibabu.

Amesema takwimu za wagonjwa hao ni takribani asilimia 20, lakini kwa mazingira ya kawaida asilimia 80 ya wagonjwa hao bado hawajafika katika vituo vya afya.

“Takwimu hizi ni asilimia 20 ambazo tunazo sisi Serikali, lakini asilimia 80 wapo wagonjwa wengi, kila familia kwa sasa kuna angalu mgonjwa mmoja, kwa hiyo tuendelee kutoa elimu,” amesema.

Mwishoni wa Januari, 2024 wataalamu wa afya na madaktari bingwa wa macho waliozungumza na Mwananchi Digital jijini Dar es Salaam, walisema wamekuwa wanapokea idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa katika hali ya ugonjwa mkali, kutokana na matumizi ya njia mbadala kutibu macho, ikiwamo matumizi ya mkojo, chumvi na vitunguu saumu.

Ugonjwa huo ujulikanao viral keratoconjunctivitis (red eyes), mbali ya Zanzibar, pia umesambaa maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

Wataalamu waliozungumza na Mwananchi Digital Januari 28, 2024 walieleza wagonjwa wanaotumia chumvi, mkojo, chai ya rangi na kitunguu saumu kama tiba, macho yao huvimba na kuuma zaidi pamoja na kupatwa homa. Athari hasi zaidi zinazotajwa ni kusababisha vidonda kwenye kioo cha jichoni.

Tiba hizo mbadala zinaelezwa zinaweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.

Daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Sarah Mrema “si kwamba wanapona wakitumia tiba mbadala, maumivu yanazidi, wakija hapa wanakuwa na maumivu makali. Ukihoji anakwambia alitumia mkojo, chumvi na njia nyingine nyingi. Unampa dawa anatumia, kisha anapona,” amesema Dk Sarah.

Daktari bingwa wa macho katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Neema Moshi amesema unapotumia vitu vikali kutibu macho, ni rahisi kuharibu kioo cha mbele cha jicho na maumivu yanayotokea huwa makali.

Via:Mwananchi.



Post a Comment

0 Comments