Tusipochukua tahadhari vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka - waziri ummy
Tusipochukua tahadhari vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka – waziri ummy
-Kila mwaka wagonjwa wa Saratani Elfu 40 wanagundulika, vifo ni Elfu 26
Na. WAF – Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa wito kwa Watanzani kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Saratani kwa kuwa kila mwaka wagonjwa wa Saratani Elfu 40 wanagundulika ambapo inapelekea vifo Elfu 26 hivyo Watanzania wasipochukua tahadhari vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vitaongezeka.
Waziri Ummy amesema hayo Februari 6, 2024 kwenye kikao cha uwekezaji na wadau wa maendeleo kwa ajili ya uanzishwaji wa kituo cha umahiri cha matibabu ya Saratani nchini kilichofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kilichofanyika Jijini Dar Es Salaam.
“Wagonjwa wanaofika hospitali ni asilimia Thelathini tu, wagonjwa wengi wapo mitaani na wanashindwa kufika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya, tunawaasa Watanzania kufika katika vituo hivyo na kupata matibabu ya Saratani ili tupunguze wagonjwa pamoja na vifo.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema kupitia mradi huo wa kuanzishwa kwa kituo cha huduma za Saratani nchini kutasaidia kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi na muda wa matibabu kwa wagonjwa.
“Nikiangalia takwimu zetu kwa mwaka 2021/22 wagonjwa 89 waliopelekwa nje ya nchi tumetumia Tsh: Bilioni 4.8 na kwa wagonjwa Saratani pekee imetumika Tsh: 3.1 Bilioni, lakini pia kufuatia kituo hiki tutaongeza huduma za tiba utalii (wagonjwa kutoka nje kuja kutibiwa Tanzania).” Amesema Waziri Ummy
Pia amesema, zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa Saratani wanaofika hospitali hali zao zinakua katika hatua ya Tatu hadi hatua ya Nne hali ambayo inapelekea kupata ugumu wa matibabu tofauti na ambavyo angewahi kujua hali yake na kuanza matibabu mapema.
“Nitoe wito kwa Watanzania wapime Saratani angalau mara moja kwa mwaka kwa kuwa Saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 25, matiti asilimia 10, tezi dume asilimia 9, mfumo wa chakula asilimia 6.5 na Saratani nyinginezo.” Amefafanua Waziri Ummy
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!