Wananchi, viongozi wamiminika katika viwanja vya Karimjee kumuaga Edward Lowassa

Wananchi, viongozi wamiminika katika viwanja vya Karimjee kumuaga Edward Lowassa.

Dar es Salaam. Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamejitokeza katika Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuaga Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyefarikia dunia Februari 10, 2024.

Lowassa alifariki katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.

Sambamba na wananchi hao, pia leo Jumanne Februari 13, 2024 wamejitokeza viongozi mbalimbali wa Serikali na wastaafu waliojitokeza katika hafla hiyo ya kumuaga Lowassa.

Viongozi ambao wameshajitokeza hadi sasa ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na wengine.

Wapo pia Mama Mariam Mwinyi, Salma Kikwete, wabunge na mawaziri wastaafu akiwemo William Ngeleja, Andrew Chenge na Mkuu wa Polisi Mstaafu, Omary Mahita.

Mbali na viongozi hao wa kisiasa,  wapo pia wasanii akiwamo Kala Jeremiah, Christina Shusho, Flora Mbasha na kikundi cha THT kwa pamoja wakiongoza nyimbo za maombolezo.

Mwili wa Lowassa unatarajiwa kuzikwa Februari 17, mwaka huu kijijini kwao Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.

Mwanasiasa huyo mkongwe alihudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kabla ya mwaka 2015 kuhamia chama cha upinzani Chadema na kisha kurejea CCM.

Via:Mwananchi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!