Afariki ghafla akichimba kaburi la bibi kizee

Afariki ghafla akichimba kaburi la bibi kizee

#PICHA:Kaburi alilokuwa akichimba Peter Simon kabla ya kufikwa na mauti  katika makaburi yaliyopo mtaa wa Mkoani Mjini Geita.

Tukio hilo la kushangaza limetokea Machi 26,2024 wakati vijana wa nzengo hiyo wakiwa makaburini wakiendelea na uchimbaji wa kaburi ndipo Peter alipata hali ya ghafla kama kifafa na kusaidiwa kwa kulazwa pembeni, lakini baada ya muda mfupi wakagundua amefariki.

Geita. Katika hali isiyo ya kawaida Mkazi wa Mtaa wa Mkoani Halmashauri ya Mji wa Geita Peter Simon(25) amefariki ghafla wakati akishirikiana na wanakijiji wenzake kuchimba kaburi  la Elizabeth Kalamu (85) aliyefariki baada ya kuugua muda mrefu.

Tukio hilo la kushangaza limetokea Machi 26,2024 wakati vijana hao wakiwa makaburini wakiendelea na uchimbaji wa kaburi ndipo Peter alipata hali ya ghafla kama kifafa na kusaidiwa kwa kulazwa pembeni, lakini ya muda mfupi wakagundua amefariki.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Geita, Thomas Mafuru amethibitisha kupokea mwili wa kijana huyo na kusema kuna sababu mbalimbali  mtu kupata kifo cha ghafla moja wapo ikiwa ni shambulio la moyo.

“Huyu kijana ameletwa na wasamaria wema hakuna ndugu yake ambaye labda angetueleza historia yake, lakini  shambulio la moyo linaweza kuwa sababu. Mtu akipata shambulio la moyo inashauriwa ujilazimishe kujikoholesha kwa nguvu ili aushtue moyo.”

Amesema pia inawezekana alikua na kifafa na alipoanguka pengine aliangukia pua na kushindwa kupumua na kuishauri jamii inapoona mtu amepata shambulio la moyo wamkalishe na kumbonyeza kwenye kifua, ili moyo uamke na kufanya kazi kama kawaida.

Mashuhuda

Katibu wa maafa katika Nzengo ya Mkoani, George Constantine amesema wakiwa kwenye msiba wa Kalamu walikwenda eneo la maziko kwa ajili ya kuchimba kaburi na wakati wakiendelea Peter alichukua jembe na kuanza kuchimba, lakini ghafla alianguka na kuonyesha dalili za mtu mwenye kifafa.

“Akiwa ameshika jembe alianguka na kuonyesha  dalili za mgonjwa wa kifafa na vijana wakaamua kumshika na kumlaza pembeni wakijua ile hali itatulia tu na atakuwa sawa, lakini baada ya kama dakika moja waliokua wanamuangalia wakasema mbona kama huyu amefariki tukamchukua na kumpeleka hospitali ndipo daktari akasema tayari amefariki”amesema Constantine.

Bakita Mgaya Mkazi wa Mtaa wa Mkoani amesema wakiwa nyumbani kwa  Elizabeth Kalamu wakiendelea na taratibu nyingine za msiba, walishangaa kuona vijana wa Nzengo wakirudi na Katibu wa maafa wakitueleza kuna kijana alikua akichimba kaburi ameanguka na amefariki.

“Hili tukio tumelipokea kwa masikitiko sana na ni la ajabu halijawahi kutokea kwenye mtaa wetu ni kijana mdogo sana. Lakini ndio hivyo tunamshukuru Mungu kwa yote maana kazi yake haina makosa”amesema Mgaya.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Paulo hili tukio ni kweli limetokea kwenye eneo langu, kuna mama alifariki jana na vijana wakaenda kutengeneza nyumba ya kumuweka na nikiwa hapa ofisini ndio nikaletewa taarifa ya kuwa kuna msiba mwingine umetokea ghafla.

“Yeye ndio alikua wa kwanza kuchimba wakati anatoa nyasi akaanza kuchimba kaburi ndio wakamuona anapepesuka wakamshika wakamlaza chini wakijua ni kifafa, lakini hakutoa mapovu nikawaambia chukueni bajaji mumkimbize hospitali lakini kabla bajaji haijafika yeye akawa ameshakufa”amesema Paulo.

Source:Mwananchi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!