Hospitali binafsi zaanza kupokea bima za NHIF

Hospitali binafsi zaanza kupokea bima za NHIF

Baada ya wagonjwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kusitishiwa huduma kwa hospitali binafsi, baadhi ya hospitali zimeanza kutangaza kurejesha huduma kwa wanachama hao.

Kiini cha wanachama wa NHIF kusitishiwa huduma, ni Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHFTA), kutangaza mgomo kikishinikiza kutokubaliana na matumizi ya kitita kipya cha mafao ya gharama za huduma 2023 kilichotolewa na NHIF, wakidai gharama zilizokokotolewa kwenye kitita hicho, ni hasara kwao.

Watoa huduma hao wamesema kama watatumia kitita kilichofanyiwa maboresho na NHIF, watakumbana na hasara ya hadi asilimia 30 kutokana na huduma nyingi kushushwa bei.

Mwenyekiti wa APHFTA, Dk Egina Makwabe ndiye aliyetangaza mgomo huo kuanzia Machi 1, 2024 kwa wagonjwa wote wanachama wa NHIF kutopokelewa kwenye hospitali binafsi, tamko ambalo lilifuatiwa na taarifa za hospitali mbalimbali kuwataarifu wanachama wa NHIF kuwa hawatapokelewa.

Hospitali ya Kairuki, Regency, T.M.J na Aga Khan ni miongoni mwa zilizotoa taarifa za kutopokea wanachama wa NHIF na baadaye NHIF ikiwaelekeza wanachama wake kutumia vituo mbadala kupata huduma, huku hospitali zinazomilikiwa na Serikali zikieleza kujipanga kupokea wagonjwa wote na kuwahudumia.

Akiwa mkoani Lindi, jana Ijumaa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliziagiza Hospitali zilizositisha kuendelea na huduma akizitaka hospitali hizo kuingia kwenye mazungumzo na Serikali.

“Kamati ya kitaalamu niliyoiunda iendelee kufanya majadiliano na watoa huduma wakati huduma zikiendelea kutolewa. Naomba kusisitiza kuwa, majadiliano yatafanyika wakati huduma zinaendelea kutolewa,”alisisitiza Ummy.

Huduma zarejea

Kutokana na tamko hilo, Hospitali ya TMJ Dar es Salaam kupitia taarifa yake kwa umma jana ilitangaza kurejesha huduma.

“Bodi ya wakurugenzi wa Hospitali ya T.M.J baada ya kusikiliza kwa umakini hotuba ya Waziri wa Afya, wizara kufungua milango ya mazungumzo, tupo tayari kufanya makubaliano na NHIF chini ya wizara wakati huduma zikiendelea kwa wanufaika na bima ya NHIF.Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza,” imesema taarifa hiyo.

Pia nayo Hospitali ya Bochi ya Dar es Salaam Machi Mosi, ilitangaza kurejesha huduma za NHIF kwa wagonjwa kama kawaida.

“Wagonjwa wa bima ya afya zingine zote wanaendelea kupewa huduma kama kawaida kauli mbiu yetu ya OKOA MAISHA KWANZA itaendelea kutumika kwa wagonjwa wa dharura,”iliandikwa kwenye taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Bochi, imewekwa na Waziri Ummy katika akauti yake ya X na kuandika, “Asanteni Bochi Hospitali na wote waliorudisha huduma kwa wanachama wa NHIF. Tunawashukuru sana sana. Ninawaahidi kuwa tutafanya maboresho katika maeneo mahususi mtakayoyaainisha ndani ya muda mfupi.”

Mbali na hizo, akaunti za kijamii za NHIF, zimeweka picha za Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga akiwa Hospitali ya Regency. Picha hizo zimeambatana na maelezo, “Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga akishuhudia kurejea kwa huduma katika Hospitali ya Regency.”

“Uongozi wa NHIF ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Bernard Konga umetembelea Hospitali ya Regency Medical Centre na kufanya mazungumzo na uongozi wa hospitali hiyo.”

Jana, baada ya kauli hiyo ya Waziri Ummy, Mwenyekiti wa APHFTA Dk Makwabe alisema wanamshukuru kiongozi huyo kwa kufungua majadiliano kwa mara nyingine.

Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa zetu, APHFTA pamoja na Serikali leo wapo kwenye mazungumzo kuondoa sintofahamu baina yao.

Chanzo: Mwananchi

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!