Idadi ya waliong'atwa na mbwa Mwananyamala yaongezeka

Idadi ya waliong’atwa na mbwa Mwananyamala yaongezeka

Idadi ya watu waliojeruhiwa na mbwa aliyekuwa akipita mtaani na kung’ata watu imefikia 28 kutoka 26 iliyokuwa awali.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Machi 11, 2024 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dk Zavery Benela, alipozungumza na kusema kuhusu maendeleo ya majeruhi walioanza kupata tiba katika hospitali hiyo siku tatu zilizopita.

Tukio hilo la mbwa kung’ata watu lilitokea Ijumaa Machi 10 ambapo mbwa huyo alikuwa akipita mtaani na kung’ata watu ovyo na kukimbia. Awali ilielezwa aliwajeruhi watoto 20 na watu wazima sita.

Dk Benela amesema majeruhi hao wapya wawili walifika hospitalini hapo leo Machi 11 na kupatiwa huduma.

“Nadhani hawa walikuwa hawajapata taarifa kwamba tunatoa huduma kwa waliopatwa na mkasa huo. Nitumie fursa hii pia kuvishukuru vyombo vya habari kwa kutufikishia ujumbe kwa wananchi.

“Nisisitize tena kwa ambaye anajua alikumbana na mbwa huyo aje kwa tutamhudumia bila malipo yoyote mpaka pale atakapomaliza tiba zote za siku saba,” amesema Mganga huyo.

Pia ameshukuru namna Halmashauri ya Kinondoni kupitia ofisi ya Mganga Mkuu ilivyokuwa bega kwa bega na wao, tangu tukio hili lilipotokea katika kuwahudumia majeruhi ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa dawa na kinga wakati wote, licha ya kuwa walitumia dawa zao za ndani lakini imewahakikishia zitakapopungua watawaongezea kwa haraka iwezekanavyo,” amesema.

Pia Dk Benela hakuisahau Wizara ya afya kwa namna ilivyokuwa haraka kupeleka sampuli maabara kupima kujua mbwa aliyehusika kama alikuwa na kichaa au la.

Kwa upande wao wazazi wa watoto waliojeruhiwa akiwemo Fatma Hamis, amesema wanashukuru kwa namna walivyohudumiwa bila ya kukaa foleni muda mrefu.

Naye Joseph Mapunda amesema kubwa wanaloshukuru ni kugharamiwa matibabu yote kwa kuwa awali ilisemekana sindano kwa ajili kinga zilizobaki wangetakiwa wajilipie ambapo kila moja iligharimu Sh32, 000 na walitakiwa kuchoma nne jambo lililokuwa likiwapa mawazo ya wapi wangepata fedha hizo.

Tayari mbwa aliyehusika kuwajeruhi watu hao aliuawa siku ya Jumamosi katika msako uliofanywa na Idara ya Mifugo ya Halmashauri ya Kinondoni. Msako huo uliwakumba mbwa wengine wawili waliokutwa wakizurura mtaani.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!