Idadi ya waliopata madhara kwa kula samaki aina ya kasa yafikia Watu 160,Vifo 9

Idadi ya waliopata madhara kwa kula samaki aina ya kasa yafikia Watu 160,Vifo 9.

Naibu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh amesema idadi ya waliopata madhara kwa kula samaki aina ya kasa Visiwani humo imeongezeka na kufikia Watu 160 huku waliofariki wakiongezeka kutoka 8 hadi 9 ambao wote ni Watoto wenye umri chini ya miaka 10.

Amesema Watu hao baada ya kula kasa katika eneo la Kisiwa Panza, Mkoa wa kusini Pemba Visiwani Zanzibar walianza kuumwa tumbo, kulegea mwili, kutapika na kuharisha na kupelewa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Abdallah Mzee Kisiwani Pemba ambapo 18 bado wamelazwa na wengine wameruhusiwa “Wizara ya afya inapiga marufuku ulaji wa kasa kutokana na kuwa na sumu kali inayotokana na vyakula wanavyokula kasa hao wakiwa Baharini, kuna aina saba ya kasa na kati ya hizo nne huwa ni hatari na wana madhara na hawafai kuliwa lakini ni vigumu kumgundua kasa mwenye sumu kati ya aina hizo saba”

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Farid Mzee Mpatani, amesema kasa ana sumu ambayo inatokana na aina ya majani na matumbawe yaliyopo Baharini na katika uchunguzi wamegundua sumu hiyo husababisha madhara katika mfumo wa ufahamu wa Binadamu na husababishwa na mimea na vimelea vya Baharini ambavyo hutumiwa na kasa kama chakula chao.

Amesema madhara ya sumu hiyo ni Binadamu kukosa nguvu, kupata ganzi, kutapika na kuharisha na kufariki dunia ambapo Watoto chini ya miaka 15 huathirika zaidi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!