GEITA YAPONGEZWA KUPUNGUZA VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA
Na. WAF – Geita
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameupongeza Mkoa wa Geita kwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya kina mama wajawazito 106,162 walijifungua huku mwaka 2023 walijifungua 116,990 lakini bila kuongeza vifo vya kina mama wajawazito.
Waziri @ummymwalimu amesema hayo leo Machi 15, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Stanslaus Nyongo katika Mkoa wa Geita ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa majengo, utolewaji wa huduma za Afya pamoja na upatikanaji wa dawa.
“Wanawake waliojifungua katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa Mwaka 2022 walikua ni 106,162 na mwaka 2023 waliojifungua ni 116,990 tunaona idadi ya wanawake waliojifungua ni wengi lakini hawajaongeza vifo vya wakina mama wajawatizo, kwa mwaka 2022 vifo vya wajawazito ni 57 na Mwaka 2023 ni vifo 55 hii ni rekodi nzuri hongereni sana.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, kutokana na taarifa ya Afya ya Mkoa inaonesha kuwa kwa mwaka 2022 kulikua na vifo vya watoto wachanga 905 ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo vifo vimepungua hadi kufikia 814, vifo hivyo vimetokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mtoto kushindwa kupumua, kuzaliwa na uzito pungufu isivyo kawaida.
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ili kuboresha huduma za Afya Mkoani Geita ikiwemo majengo, vifaa tiba pamoja na dawa ambapo kwa sasa ujenzi wa jengo la huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita unaendelea ambalo utagharimu kiasi cha fedha Tsh: Bilioni 13 likiwa limefikia asilimia 50 ili kumalizika kabla ya Disemba 2024.
“Kwa kipindi cha miaka Mitatu ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Geita umepokea Jumla ya Mashine za X-ray 13 ambazo zimefungwa na kutoa huduma kwa wananchi na hivyo kuufanya Mkoa huo kuwa na Jumla ya Mashine za Mionzi 20.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema uwepo wa mashine hizo umepunguza Rufaa za wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali ya Bugando kwa kiwango kikubwa ambapo katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 jumla ya wananchi 8,314 walipata huduma ya kipimo cha X-ray, wananchi 343 walipata huduma ya kipimo cha CT Scan na wananchi 28 huduma za MRI.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!