Bilionea Sabodo afariki dunia, atakumbukwa miaka ya 1970 nchi ilipokumbwa na uhaba wa mafuta alimuomba Mwalimu Nyerere kwenda Iran kuomba mafuta, pia alikuwa mfadhili wa vyama vya Chadema na CCM, alichimba visima zaidi 280 nchi nzima.
Bilionea mzaliwa wa mkoani Lindi, Mustafa Sabodo amefariki dunia. Atakumbukwa kwa uzalendo wake ambaye nchi ilipokumbwa na uhaba wa mafuta miaka 1970, alikwenda kwa Ayatollah Khomeini nchini Iran kuomba nishati hiyo.
Pia, Sabodo atakumbukwa kwa ufadhili wake kwa vyama vya CCM na Chadema, misaada kwa jamii na aliwahi kutangaza kutoa Dola 5 bilioni za Marekani (Sh10 trilioni), kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli kuhamishia Serikali mkoani Dodoma.
Sabodo mwenye asili ya Asia aliyezaliwa mwaka 1942 mkoani Lindi, ni bilionea ambaye biashara zake zimesambaa kwenye nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, India, Ufaransa, Kenya, Sudan na Zimbabwe.
Kifo cha Sabodo kimetangazwa na mtoto wake Danstan kwamba amefariki dunia leo Machi 23, 2024 alfajiri akiwa nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam.
Sabodo ambaye ametoka kwenye familia ya Uislamu wa Kihindi wa Gujarati Khoja, atakumbukwa kwa moyo wake wa kupenda kusaidia watu, uzalendo, kupenda demokrasia na maendeleo.
Misaada aliyotoa kwa jamii ya Watanzania, imefanya jina lake kuwa maarufu kwenye mioyo ya wananchi wengi, pia kwa kupenda kwake demokrasia anatajwa kuvifadhili vyama vya siasa vya CCM na Chadema kwa nyakati tofauti.
Sabodo katika maisha yake alimpenda Mwalimu Nyerere na alikuwa rafiki yake wa karibu na katika miaka 1970, nchi ilipokumbwa na uhaba wa mafuta alimuomba Mwalimu Nyerere amruhusu aende nchini Iran kukutana na Kiongozi wa taifa hilo, Ayatollah Khomeini kwa ajili ya kuomba mafuta.
Uhaba huo wa mafuta ulisababisha Serikali kuzuia magari kutembea Jumapili, huku Jumamosi yakitembea hadi saa nane mchana.
Kwa mujibu wa mahojiano aliyowahi kufanya na vyombo vya habari, Sabodo alisema; “Nikamwambia wacha niende Iran. Nilifanya hivyo nikiamini Khomeini atanisikiliza. Nakumbuka nilikwenda na Chifu Adam Sapi Mkwawa.
“Mimi ni Khoja, Mwislamu wa dhehebu la Shia na Khomeini pia, nilipokutana naye, nikamwambia wanavyoteseka Tanzania kwa shida ya mafuta wamo pia Waislamu wa Shia wengi tu.”
“Nilimwambia Tanzania ni nchi nzuri haina ubaguzi na Rais Nyerere ni mtu mwema, hata Waziri Mkuu wake ni Rashid Kawawa na Waziri wa Madini na Mafuta ni Anoor Kassam, nikamwangukia miguuni nikilia kuomba aipe nchi yetu mafuta, akakubali.”
Kwa mujibu wa Sabodo, Khomeini alimtaka viongozi wa Serikali ndio waende kupewa mafuta na si yeye kama Sabodo.
“Nikarudi Tanzania na kumpa taarifa baba wa Taifa naye alimwambia Kawawa na John Malecela ikakubalika tukaenda tena Iran safari hii nikiwa na mawaziri wa Fedha, Cleopa Msuya, Anoor Kassam wa Mafuta na Usafirishaji pia alikuwepo Peter Noni kwa niaba ya Benki Kuu na Adam Sapi Mkwawa,” alisema.
Sabodo alikumbuka kuwa safari hiyo ilizaa matunda kwani Khomein aliipa Tanzania mafuta yenye thamani ya Dola 80,000 za Marekani.
“Nakumbuka hapo urafiki wangu na Nyerere uliniwezesha kuliokoa Taifa kwa kupata mafuta baada ya kunituma kwenda Iran nilipomshauri,” alisema.
Pia, Sabodo kwenye safari hiyo alimshauri Khomeini kufungua ofisi ya ubalozi wa Iran nchini naye alikubali na alifanya hivyo pia kwa Zambia, Tanzania nayo ikafungua ubalozi Iran.
Moyo wa kujitolea
Sabodo licha ya kuwa mwanachama wa CCM, alitoa Sh100 milioni kwa ajili ya kukipongeza chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa ajili ya ushindi wa kiti cha ubunge alichoshinda Joshua Nasari wa jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha wakati huo.
Pia, alitoa baiskeli 100 na kuahidi kuchimba visima vitano katika jimbo hilo.
Mwaka 2003, Sabodo alitoa udhamini wa uchezeshaji wa bahati nasibu ya mfuko wa Mwalimu Nyerere wenye thamani ya Sh100 milioni.
Wazo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa Mwalimu Nyerere lilikuwa la Sabodo, pia alichangia Sh1.3 bilioni katika kuufanikisha.
Pia, Sabodo amechangia miradi mbalimbali ikiwemo kutoa kiasi cha Sh5 bilioni kwa ajili ya kuchangia chuo cha ualimu cha elimu ya juu cha Mtwara, alichangia Sh965 milioni kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya Hospitali ya Shree Hindu Mandal, mradi wa Khoja Shia-aheri Sh6 bilioni.
Licha ya kupooza sehemu ya mwili wake mwaka 2000, Sabodo aliendelea kufanya kile anachotaka ikiwemo kusimamia miradi yake na ya jamii kuhakikisha inafanikiwa, ikiwamo kuchimbia visima zaidi ya 280 nchini.
Kumuunga mkono Magufuli
Sabodo alitangaza kutoa Dola5 bilioni za Marekani (Sh10 trilioni) kwa ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya Serikali kwenda mkoani humo.
Kwa mujibu wa Sabodo uwekezaji huo ulikuwa na sharti la Serikali kuhamia Dodoma kwa kuwa Magufuli atakuwa ametimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.
“Niliposikia anatangaza kwenye televisheni ya Taifa kwamba Serikali itahamia Dodoma, ilikuwa mara yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita, nilitabasamu moyoni, jambo ambalo lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona ile roho ya Nyerere imezaliwa tena.
“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la Dodoma kwa kuwekeza Dola za Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” ilikuwa ni kauli ya Sabodo ambaye sasa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa Sabodo fedha hizo zililenga kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.
Elimu yake
Kielimu, Sabodo alisoma Shule ya Sekondari ya Lindi na baadaye alihitimu ngazi ya cheti kwenye Chuo cha Cambridge.
Baadaye alihitimu Chuo cha Edinburg nchini Uingereza mwaka 1965 ambapo alisoma sheria ya biashara na usimamizi wa mifuko ya fedha.
Source:Mwananchi.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!