Wataalam wa optometria watakiwa kujisajili kwenye mfumo wa usajili wa wataalam (hprs)

Wataalam wa optometria nchini watakiwa kujisajili kwenye mfumo wa usajili wa wataalam (hprs) ili waweze kutambulika

Na WAF – Dodoma

Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastiano G. Millanzi amewataka wataalam wa kada ya Optometria waliohitimu mafunzo yao kutoka vyuo vya Mvumi, KCMC na nje ya nchi kuhakikisha wanajisajili katika mfumo wa _Health Practitioner Registration System_ utakaowawezesha kutambulika katika mifumo mingine ya Serikali.

Millanzi ametoa rai hiyo Machi 22, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya wataalam wa Optometria waliohitimu vyuo na wanaotarajia kutoa huduma ya macho yanayofanyika kwa siku moja jijini hapo yenye lengo la kuwafanya wataalam kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili pamoja na utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Millanzi amesema uwepo wa Baraza hilo unatambuliwa kupitia Sheria ya Bunge ya Mwaka 2007.

“Baraza ni ndio chombo pekee nchini chenye dhamana ya kutoa Leseni za wataalam wa Optometria na kuzisimamia, kwa wale waliosoma vyuo vya ndani na nje ya nchi, hivyo kila muhitimu wa kozi hiyo ili aweze kutekeleza majukumu yake lazima apate usajili wa Baraza hilo”. Amesema ndugu Millanzi.

Millanzi amefafanua kuwa, lengo la sheria husika ni kutumika kudhibiti ubora wa huduma zitolewazo na wataalam hao na kwa mujibu wa kifungu cha 11 kinachohusu sifa za mtaalam kupata usajili wa baraza.

Akiwasomea baadhi ya sheria zinazo simamia watoa huduma, Naibu Msajili Ramadhani Msuya kutoka baraza hilo, amesema mtaalam yeyote atakaye kwenda kinyume ataadhibiwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamia taaluma hiyo.

“Tumezoea kuona watu wanauza miwani mtaani lakini hilo ni kosa kisheria kwani kupitia kifungu cha 40 (1) ataweza kushtakiwa na kuadhibiwa au faini yake kufikia hadi Sh. milioni kumi au kifungo cha miaka mitano ama vyote viwili kwa pamoja.

Kwa upande wao wataalam hao, wamesema watakuwa tayari kufanya kazi kwa weledi ili kulinda hadhi ya taaluma.

“Kazi hii ni lazima uwe muadilifu, hivyo nitahakikisha ninatunza siri za mgonjwa nikiwa mtoa huduma niliye hitimu mafunzo yangu ambayo yananitaka kufanya hivyo”. Amesema Bi. Digna Kakazoka ambaye ni muhitimu wa kada ya optometria kutoka chuo cha KCMC mkoani Kilimanjaro.

Jumla ya wataalam 32 wamepatiwa usajili wa kudumu na jumla ya wataalam 44 wamepatiwa usajili muda ambapo watatakiwa kutoa huduma katika vituo vinavyotambuliwa na baraza chini ya uangalizi wa Mtaalam wa Optometria au Madaktari Bingwa wa Macho mzoefu.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!