Wizara ya afya ipo katika mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007

Wizara ya afya ipo katika mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007.

 Waziri Ummy Mwalimu amesema mazungumzo ya NHIF na watoa huduma za afya yanaendelea, wiki hii anatarajia kupokea ripoti ya kilichozungumzwa na mwafaka uliofikiwa.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wizara ipo katika mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 katika kuboresha sekta ya afya.

Amesema uboreshaji utaimarisha ubora wa huduma za afya, ugharamiaji huduma na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema watatoa elimu kwa wananchi kuhusu mtindo bora wa maisha.

“Tunataka tukirudi kwenye maadhimisho ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan mtupime kwenye huduma za afya, kwani tunataka zifanyike kwenye ubora uliokusudiwa, maana tunaweza kuwa na miundombinu lakini utendaji kazi na lugha zetu hazifai,” amesema.

Akizungumza leo Jumatano Machi 27, 2024 kwenye kongamano la Kurasa 365 za Mama Samia lililoandaliwa na Clouds Media, Ummy amesema sera inayoandaliwa ina dira ya kuwa na jamii yenye afya bora na ustawi, inayochangia kikamilifu katika maendeleo binafsi na ya nchi.

Amesema Serikali inalenga kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kupunguza rufaa za wagonjwa za nje ya nchi na kuvutia wagonjwa kutoka nje.

Kwa kuzingatia dira ya Taifa ya maendeleo, mpango mkakati wa sekta hiyo amesema ni kuendelea kufanya uwekezaji kwenye huduma ya afya ili kufikia lengo la afya kwa wote.

Pia kuhakikisha kila mwananchi anakuwa katika mfumo wa bima ya afya kwa kuimarisha huduma ya kinga na tiba.

“Tatizo lililopo hapa ni ubora wa huduma kwani wanaoenda kwenye hospitali za binafsi wanatibiwa na madaktari wa Serikali lakini tatizo lililopo ni lugha inayotumika,” amesema.

Wizara itaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha mifumo ya ugharimiaji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kikwazo cha fedha, ikiwemo kuanza utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Amezungumzia pia kuimarisha Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), akiwataka watoa huduma ya bima ya afya binafsi kuanzisha vifurushi vitakavyowasaidia wananchi.

Amesema ili kufikia malengo hayo, mazungumzo ya NHIF na watoa huduma yanaendelea na wiki hii anatarajia kupokea ripoti ya kilichozungumzwa na mwafaka uliofikiwa.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kufikia lengo la asilimia 95 ya wanaojifungulia kwenye vituo vya afya ifikapo mwaka 2030.

Amesema idadi ya wanaojifungulia vituo vya kutolea huduma za afya imeendelea kuongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2021 hadi asilimia 85 mwaka 2023.

Waziri Ummy amesema watahakikisha wanapunguza vifo vya watoto kwani fedha zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa wodi maalumu kwa ajili ya kuhudumia watoto wachanga kuanzia umri 0 hadi siku 28.

Amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita wameongeza vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia 9,610 Machi 2024 sawa na ongezeko la vituo 1,061.

Pia wamejenga majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mitano, uboreshaji huo ukigharimu Sh1.02 trilioni.

“Tumekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara, awamu ya pili ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Chato,” amesema Ummy.

Pia wameendeleza ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa ya Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita na tayari zimeanza kutoa huduma.

Katika huduma za vipimo, amesema kwa sasa CT-Scan zinapatikana katika hospitali 27 kati ya hospitali 28 za rufaa za mikoa nchini.

Amesema kwa mwaka 2023 jumla ya wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo hicho.

Ili kuhakikisha wagonjwa hawakosi vitanda, amesema wameongeza idadi ya vitanda kutoka 86,131 mwaka 2021 hadi 126,209 Machi, 2024.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!