KENYA:Kifo cha Jenerali Ogolla kinaacha ombwe katika nafasi hiyo nyeti ya ulinzi wa Taifa

Kifo cha Jenerali Ogolla kinaacha ombwe katika nafasi hiyo nyeti ya ulinzi wa Taifa, Rais Ruto na Baraza la Ulinzi wanatarajiwa kumteua mrithi.

Nairobi. Jenerali Francis Omondi Ogolla amekuwa mkuu wa kwanza wa vikosi vya ulinzi nchini Kenya kufariki dunia akiwa madarakani, baada ya ajali ya helikopta iliyoua wanajeshi 10 wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

Rais wa Kenya, William Ruto usiku wa Alhamisi Aprili 19, 2024 alithibitisha vifo hivyo, akitangaza siku tatu za maombolezo na bendera kupepea nusu mlingoti. Tukio hilo linatokea kwa mara ya kwanza kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kufariki dunia akiwa madarakani nchini Kenya.

Kufariki kwa Ogolla kunasababisha Baraza la Ulinzi la nchi hiyo kumchagua mrithi wa nafasi hiyo nyeti katika ulinzi wa Taifa. Anaweza kutoka katika kamandi ya wanaanga kama ilivyokuwa kwa Ogolla au kamandi ya wanamaji kwa kufuata mzunguko wa madaraka chini ya sheria ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 23 cha Sheria ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi huteuliwa na Rais kwa mapendekezo ya Baraza la Ulinzi.

Baraza hilo kwa mujibu wa Kifungu cha 241 cha Katiba, linajumuisha Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na makamanda watatu wa Majeshi ya Ulinzi.

Hayati Jenerali Ogolla aliyeteuliwa mwaka mmoja uliopita kushika wadhifa huo alitarajiwa kustaafu mwaka 2025.

Kutokana na sheria ya ulinzi nchini humo, wanaotajwa huenda watakuwa warithi wa Ogolla ni pamoja na Meja Jenerali John Mugaravai Omenda kwa sasa ndiye Kamanda wa Kamandi ya Anga na Meja Jenerali Thomas Njoroge Ng’ang’a ambaye ni Kamanda wa Kamandi ya Wanamaji.

Ajali za helikopta zinavyotikisa Kenya

Ajali ya helikopta iliyomuua Mkuu wa Majeshi Kenya si ya kwanza kutokea.

Juni 2021: Eneo la Kajiado Magharibi ilitokea ajali kama hiyo, wanajeshi 10 wa KDF walifariki dunia na 13 walijeruhiwa.

Mei 2021: Ajali ya helikopta iliyombeba kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga ilitokea lakini hakukuwa na kifo, rubani na abiria mmoja walipata majeraha madogo.

Januari 2021: Ajali ya helikopta ya Kamandi ya Anga Kenya ilitokea katika Hifadhi ya Taifa ya Tsavo, hakukuwa na madhara makubwa.

Oktoba 2020: Ajali ya helikopta ilitokea Kaunti ya Narok, Gavana Samuel Ole Tunai alikuwa ndani, lakini hakukuwa na madhara.

Oktoba 2017: Ajali ilitokea Ziwa Nakuru, baadaye iligundulika kuwa rubani alikuwa amelewa, pia hakukuwa na madhara makubwa katika ajali hii.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!