Mwili uliozuiliwa Bugando kisa deni la Sh18 milioni wazikwa

Mwili uliozuiliwa Bugando kisa deni la Sh18 milioni wazikwa

Hatimaye mazishi ya marehemu Juma Jumapili (60) ambaye mwili wake ulizuiwa kutolewa kwa siku kadhaa katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Jijini Mwanza akidaiwa Sh18 milioni kama gharama za matibabu yamefanyika jana Aprili 5, 2024 mkoani Simiyu.

Mazishi hayo yamefanyika katika makaburi ya familia yaliyoko eneo la Sakwe wilayani Bariadi.

Marehemu Jumapili aliyepata ajali ya pikipiki Desemba 2023 na alifikishwa kupatiwa matibabu kwa mara ya kwanza hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Somanda na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu iliyoko Nyaumata na pia kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.

Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya kufikiwa kwa mwafaka wa deni hilo lililokuwa likidaiwa na hospitali hiyo tangu Aprili 1, 2024 hadi wanafamilia walipotoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga wakiomba msaada wa kupewa mwili wa ndugu yao.

DC Simalenga aliwasaidia ndugu hao baada ya kupokea kilio chao alipofanya ziara Katika kata ya Ikindilo na baadaye kufanya mkutano wa hadhara eneo la Sakwe.

“Hivyo ndugu zangu nawaombeni mje ofisini kwangu nitawaandikia barua ya kuwatambulisha na kutoa maelekezo kama Serikali ili muweze kuupata mwili wa ndugu yenu, kwa kuwa ni maelekezo ya Rais kuwa ndugu asishindwe kumuhifadhi ndugu yake kwa sababu ya deni analodaiwa na hospitali,” alisema Simalenga.

Akitoa maombi katika mkutano huo, kaka wa marehemu, Elias Jumapili alisema wamehangaika kupata mwili wa ndugu yao kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha.

“Tumekuwa tukihangaika namna ya kuupata mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi changamoto ni kukosa pesa ambazo Hospitali ya Bugando umeeleza ni gharama zilizotumika kwenye matibabu yake,” alisema.

Wakizungumza na Mwananchi baada ya kufanyika kwa mazishi hayo, wanafamilia wameelezea changamoto walizopitia baada ya ndugu yao kupata ajali ya pikipiki aliyokuwa akiendesha, hadi mauti yalipomfika.

Mwali Jumapili ambaye ni ndugu wa marehemu ameeleza kuwa walilazimika kuuza ng’ombe, mashamba na baadhi ya vitu vya thamani ikiwa ni hatua za kugharamia matibabu yake.

“Ndugu yetu alipata ajali ya bodaboda akiwa anaendesha yeye mwenyewe na alipata majeraha makubwa kichwani na maeneo mengine ya mwili, akapelekwa hospitali ya Somanda iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kabla ya kuhamishiwa Bugando kwa matibabu zaidi,” amesema.

Akieleza historia fupi ya marehemu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwagala, Elias Mganga amesema kuwa marehemu alikwenda Bariadi mjini kutafuta maisha akifanya ufundi wa baiskeli na alipata ajali hiyo iliyosababisha kifo chake.

Ameeleza kuwa baada ya mazungumzo, Hospitali ya Bugando wameondoa baadhi ya gharama na kuwataka walipe Sh8 milioni.

Chanzo: Mwananchi

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!