Tuepuke tabia bwete kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza

TUEPUKE TABIA BWETE KUKABILIANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA.

Na WAF – DODOMA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaasa watumishi wa umma, binafsi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanaepukana na tabia bwete ili kukabilina na Magonjwa yasiyoambukiza.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ametoa rai hiyo wakati kikao cha Makatibu Wakuu kilicholenga kujadili afua jumuishi za kuzuia na kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza April 5, 2024 ambapo amezisihi Wizara za kisekta na wadau kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuja na ajenda ya kitaifa juu ya kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza.

“Tuhamasishane kuanzia maofisini kuacha tabia bwete na tuwe na hulka ya kufanya mazoezi, tuwe na siku maalum ya matembezi kwenda kazini, Mfano, Wizara ya Afya kwa wiki itenge siku tatu za kufanya mazoezi jioni. Hii itatufanya kuwa na Afya bora“. Amesema Dkt. John Jingu.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa wizara na sekta ya afya kufikiri mbali zaidi na kuunda mikakati madhubuti ya kuhamasisha watanzania kubadili mitindo wa maisha.

“Tufikirie zaidi na kuja na afua madhubuti zitakazo hamasisha watanzania kubadili mitindo ya ulaji wenye mantiki, kwani Vyakula vyenye lishe vinapatikana kwenye maeneo yetu na kwa urahisi Kama mboga za majani, tuache kupendelea vyakula vya fast food” Amesema Dkt. Jingu.

Akizunguza kwenye kikao hicho Daktari bingwa na katibu wa chama cha magonjwa yasiyoambukiza Prof. Kaushik Ramaiya amesema lazima jamii ijue magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuzuilika kwa kutoa elimu kwa jamii ili wabadilishe mitindo ya maisha yao kwa kuzingatia mazoezi na ulaji wa vyakula vyenye lishe bora.

Awali akitoa wasilisho Mtaalam wa Sheria za Afya Bw. Augustus Fungo amesema ili kuweza kudhibiti ulaji vyakula vyenye sukari, chumvi na mafuta, Serikali itaendele kutilia mkazo uwekwaji wa taarifa sahihi katika vifungashio vya vyakula, kumpa machaguo mwananchi huku akitilia mkazi kwa serikali kuunda sheria kuongeza kodi kwenye vinywaji vyenye sukari, chumvi nyingi ili kupunguza matumizi ya vitu hivyo.

“Vyakula tunavyonunua kwenye maduka ya bidhaa za vyakula hawaweki taarifa za vitu vilivyotumika kwenye kutengeza vyakula hivyo , hivyo serikali ikitilia mkazo kwenye hili litampa machaguo mwananchi pale anapoona kuwa chakula kina mafuta, sukari au chumvi nyingi, pia kuongeza pei ya kodi ya vinywaji wenye sukari hii itafanya vinywaji hivyo kiuzwa kwa bei ya juu sokoni na kumfanya mwananchi kutotumia vinywaji hivyo”.
Amesema Bw. Fungo.

Mwisho.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!